Katika kuadhimisha siku ya mionzi duniani Halmashauri ya Mji Njombe imezindua huduma za mionzi katika kituo cha Afya Ihalula jengo ambalo limegharimu kiasi cha shilingi milioni 92.6 ambapo Halmashauri imechangia kiasi cha shilingi milioni 90.6 na nguvu za Wananchi milioni 2.
Akiwasilisha taarifa ya ujenzi wa jengo la mionzi Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Ihalula amesema kuwa kuanza kwa huduma hiyo ya mionzi kutapunguza gharama na umbali kwa Wananchi kutafuta huduma ya mionzi na jumla ya wakazi elfu kumi na mbili mia tisa tisini na nne (12,994) wanatarajiwa kunufaika na huduma ya mionzi katika kituo hicho.
Akizungumza na Wananchi waliofika kupata huduma katika Kituo cha Afya Ihalula Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Njombe Erasto Mpete amesema kuwa kwa sasa huduma zote muhimu za ultra-sound, x-ray zimeanza kupatikana katika kituo hicho rasmi na hivyo hakuna haja ya kwenda katika vituo vya afya vingine kupata huduma hizo.
"Niwaombe Wananchi kutumia fursa ya kituo cha Afya Ihalula kuchangamkia fursa za kibiashara kwa kuanzisha maduka ya kisasa, hoteli na nyumba za kulala wageni ili Wananchi watakaokuja kupata huduma kituoni hapo wasikose malazi au huduma muhimu za madukani."Alisema Mpete
Mwenyekiti wa huduma za Jamii Halmashauri ya Mji Njombe Angela Mwangeni ameishukuru Serikali kwa kusogeza huduma katika Kituo hicho ambacho awali Wananchi walilazimika kwenda Uwemba na Mjini Njombe kupata huduma za afya.Mwangeni amesema kuwa kwa sasa kazi iliyosalia ni kuhakikisha kuwa vituo hivyo vinatumika na pia kuweka matumaini kwa Serikali ya Chama Cha Mapinduzi kwa hatua kubwa waliyoifanya.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Njombe Kuruthum Sadick amewaahidi Wananchi kuwa atahakikisha kuwa anatafuta Wataalamu wa Chumba cha kuhifadhia maiti ili kuendelea kuimarisha huduma kituoni hapo na pia kupitia mapato ya ndani ya Halmasahuri kutenga fedha kwa ajili ya ununuzi wa jenereta kubwa na la kisasa litakalowezesha kuendesha shughuli zote kituoni hapo.Kwa upande wao baadhi ya Wananchi waliofika kupata huduma katika Kituo hicho akiwemo Benno Msemwa na Katarina Lupenza wamesema kuwa huduma zinazotolewa ni za kisasa na pia imewarahisishia kupunguza gharama za kusafiri na muda wa kutafuta huduma
Ofisi yetu inapatikana barabara ya Njombe-Songea mtaa wa Mjimwema.
Sanduku la Posta: S.L.P 577
Simu ya Mezani: 026-2968833
Simu ya Mkononi: 026-2968833
Barua Pepe: td@njombetc.go.tz
Haki Miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Njombe