Mkuu wa Wilaya ya Njombe Njombe Mhe. Kissa Kasongwa Aprili 17, 2024 aliiongoza Kamati ya Ulinzi na Usalama ya wilaya pamoja na menejimenti ya Halmashauri ya Mji Njombe kutembelea shamba la mkulima bora wa zao la parachichi kwa lengo la kujifunza mbinu za kisasa katika uzalishaji wa zao hilo.
Shamba hilo linalomilikiwa na Bwana Frank Msuya linalofahamika (HAVILA FARM) lililopo kijiji cha Nundu kata ya Yakobi mjini Njombe lina ukubwa wa zaidi ya hekari 200 na miti zaidi ya elfu 10 ya parachichi aina ya Hasi.
Akiwa shambani hapo, Mhe. Kissa amepongeza mkulima huyo kwa uwekezaji mkubwa na matumizi ya teknolojia kwenye kilimo cha zao la parachichi aina ya HASI ambayo ni dhahabu ya kijani inayopatikana mkoani Njombe.
Kwa upande wake Bw. Frank ameishukuru Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha umeme kufika eneo la uwekezaji jambo lililompunguzia gharama za kuhudumia shamba haswa kwenye upatikanaji wa maji.
“Parachichi inahitaji maji, Uwepo wa nishati ya umeme umenirahisishia kumwagilia mazao yangu kwa urahisi ambapo mwaka jana nilliweza kuvuna tani 80 za parachihi,” alisema na kuongeza kuwa utoaji wa ruzuku kwenye mbolea na upatikanaji wa bure wa homoni kwa ajili ya wadudu waharibifu kwenye zao la parachichi inayotolewa na serikali umesaidia kukua kwa kilimo cha zao la parachichi.
Bw.Frank alianza kilimo cha parachichi mwaka 2007, kutokana na matumizi bora ya teknolojia na mavuno yameongezeka kutoka tani 4 hadi 80 mwaka 2023.
Ofisi yetu inapatikana barabara ya Njombe-Songea mtaa wa Mjimwema.
Sanduku la Posta: S.L.P 577
Simu ya Mezani: 026-2968833
Simu ya Mkononi: 026-2968833
Barua Pepe: td@njombetc.go.tz
Haki Miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Njombe