Na.Ichikael Malisa.
TAREHE 17,Novemba 2024 Halmashauri ya Mji Njombe imeadhimisha Siku ya Watoto Njiti duniani kwa mara ya kwanza, ikiwa ni juhudi za kuhamasisha na kutoa elimu kwa jamii kuhusu umuhimu wa kuwajali na kuwaheshimu watoto wanaozaliwa kabla ya kutimiza wiki 37 za ujauzito (njiti) na wenye uzito pungufu.
Akizungumza wakati wa Hafla hiyo iliyofanyika katika hospitali ya Mji Njombe Kibena ,Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo Dr. Ayub Mtulo,alisema lengo la kufanyika maadhimisho hayo ni kutoa elimu kwa jamii kuhusu watoto njiti na haki zao.
"Lengo la maadhimisho haya ni kutaka jamii kutambua kuwa watoto njiti wapo na wanaishi. Lazima tuwaheshimu, tuwatunze, na kuwathamini. Pia, tunatoa elimu kwa jamii kuhakikisha kuwa hakuna unyanyapaa dhidi ya akinamama wanaojifungua watoto njiti."
Alitoa wito kwa wazazi hasa wanaume kuachana na dhana potofu kuhusu watoto njiti akiwataka wanaume na akina mama kushirikiana katika malezi ya watoto hao ili kufanikisha ukuaji wao.
Aidha, alieleza kuwa hospitali Mji Njombe Kibena imepiga hatua kubwa katika kuboresha huduma kwa watoto njiti.
“Hospitali yetu ilikuwa na chumba kidogo sana. Lakini sasa tuna jengo jipya linalokidhi vigezo vyote, vifaa vya kisasa na kwa umuhimu wa watoto hawa tumeweka wataalamu wa kutosha ambao wanahudumia kitengo cha watoto njiti peke yake tofauti na mwanzoni. Malengo yetu ni kupunguza vifo vya watoto wachanga na watoto njiti.”
Alisisitiza jamii kuwajali wajawazito, kuwahimiza kuhusu lishe bora, na kuhakikisha wanapata huduma bora kabla, wakati, na baada ya kujifungua.
Maadhimisho ya siku ya watoto Njiti dunia 2024 yameongozwa na kaulimbiu inayosema, Kitendo kidogo,matokeo makubwa ikielezea umuhimu wa wazazi kutumia njia ya Kangaroo kusaidia ukuaji wa watoto Njiti.
Ofisi yetu inapatikana barabara ya Njombe-Songea mtaa wa Mjimwema.
Sanduku la Posta: S.L.P 577
Simu ya Mezani: 026-2968833
Simu ya Mkononi: 026-2968833
Barua Pepe: td@njombetc.go.tz
Haki Miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Njombe