Halmashauri ya Mji Njombe Leo imeanza mafunzo ya siku mbili kwa Waheshimiwa Madiwani lengo ikiwa ni kuwajengea uwezo kwenye utendaji kazi wao na kuweza kutoa huduma nzuri kwa Wananchi kwa kuzingatia utawala bora wa sheria.
Akifungua mafunzo hayo Mkuu wa Wilaya ya Njombe Kissa Gwakisa ameipongeza Halmashauri kwa kuweza kuandaa mafunzo hayo na amewataka Waheshimiwa Madiwani kuwa Wasikivu kwa kile watakacho fundishwa na Wakufunzi kwani kile kitakacho fundishwa ni muhimu sana kwao kwa sababu itawasaidia kufanya kazi zao za uongozi kwa weledi na kuwashirikisha Wataalam na Wananchi kwa ujumla.
“Niwapongeze kwa hatua hii na ni jambo jema la kuigwa na Halmashauri nyingine kutoa mafunzo kwa Madiwani. Mafunzo ni jambo zuri kwani linatuongezea maarifa ya mambo mapya na pia kutukumbusha pale ambapo tulikuwa tumesahau. Tukumbuke kuwa kila Diwani atathaminiwa endapo atakua anatekeleza majukumu yake kwa weledi na ufanisi hivyo kwa yale yote ambayo yatakayofundishwa kupitia mafunzo hayo kila Diwani anapaswa kuyazingatia” Alisema Kissa
Awali akitoa taarifa fupi ya lengo la mafunzo hayo Mkuu wa Idara ya Utumishi na Utawala Halmashauri ya Mji Njombe Ester Gama amesema kuwa ili kuwa na uelewa wa pamoja na kufanikisha uendeshaji wa shughuli za Halmashauri kwa ufanisi kati ya Waheshimiwa Madiwani na Watendaji ndio maana idara hiyo iliona umuhimu wa kuandaa mafunzo hayo ambapo pia kwa siku ya ijumaa Halmashauri imeandaa mafunzo kwa Wenyeviti wa Mitaa na Vijiji vyote ndani ya Halmashauri ili kuweza kukumbushana wajibu wao kwenye utekelezaji wa majukumu yao ya uongozi.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Njombe Kuruthum Sadick amesema kuwa Halmashauri imeweza kufanikisha mafunzo hayo kwa kutumia rasilimali zake hivyo kila Diwani anatakiwa kuona umuhimu wa mafunzo hayo yatakayowezesha utendaji kazi wa ufanisi wa majukumu yao.
“Ili Halmashauri yetu iweze kuwa bora tunahitaji pia umoja na ushirikiano kuafnya kazi kwa kusaidiana na kukosoana pale ambapo tunakua tunakwenda tofauti ili wote twende pamoja. Mafunzo ni jambo moja lakini utekelezaji wa kile tulichojifunza ndio cha msingi na ambacho tunapaswa kukizingatia.”Alisema Mkurugenzi
Stephen Mutambi Mkurugenzi Msaidizi Utawala Bora na Maendeleo ya Jamii Ofisi ya Rais TAMISEMI ambaye ni miongoni mwa Wakufunzi wa Mafunzo hayo kwa Madiwani amesema kuwa ni vyema kila Diwani kuhakikisha kuwa anakuwa na desturi ya kuwa na utawala wa kisheria ,kufanya kazi kwa uwazi na uadilifu na pia kuhakikisha Wananchi wake wanakua na taarifa sahihi juu ya masula mbalimbali ikiwemo mapato na matumizi haya yote ikiwa ni kuwezesha utawala bora kwenye jamii wanayoihudumia.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti tofauti Diwani wa Viti Maalumu Kata ya Njombe Mjini Tumaini Mtewa amemshukuru Mkurugenzi na kuandaa mafunzo hayo ambayo yanawaongezea maarifa zaidi katika shughuli zao za uongozi na pia kuwakumbusha wajibu wao katika kuwahudumia Wananchi.
Tumaini aliendelea kusema kuwa mafunzo hayo pia yameweza kuwaeleza wajibu wao wa kuhakikisha kuwa wanaisemea Serikali na Wananchi wanakuwa na uelewa wa shughuli zinazoendelea na zinazofanywa kwenye Kata zao.
“Mafunzo haya yamekuwa na umuhimu sana mfano kwa sasa katika kipindi hiki ambacho Halmashauri imepokea fedha za ujenzi wa madarasa hivyo ni jukumu leo kuhakikisha kuwa tunawaambia Wananchi” Alisema Tumaini
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Njombe Erasto Mpete amewashukuru Wakufunzi kuwa na mada ambazo moja kwa moja zinalenga kwenye utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku na pia amesema kuwa yeye na timu ya Madiwani wa Halmashauri ya Mji Njombe wapo tayari kusikiliza na kutekelza yale yote yatakayokuwa yamefundishwa kwa muda wa siku mbili na kuyatumia kwa ustawi wa Halmashauri
Ofisi yetu inapatikana barabara ya Njombe-Songea mtaa wa Mjimwema.
Sanduku la Posta: S.L.P 577
Simu ya Mezani: 026-2968833
Simu ya Mkononi: 026-2968833
Barua Pepe: td@njombetc.go.tz
Haki Miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Njombe