Disemba 17,2024 ,Madiwani wa Halmashauri ya Mji Njombe wakiongozwa na Mwenyekiti, Mheshimiwa Erasto Mpete, wamefanya ziara ya utalii wa ndani katika Hifadhi ya Taifa ya Tarangire baada ya kukamilisha ziara ya mafunzo katika Manispaa ya Moshi.
Ziara hiyo ni sehemu kuunga mkono kampeni ya Mheshimiwa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kupitia filamu ya Royal Tour kutangaza na kuendeleza utalii wa ndani nchini Tanzania.
Mheshimiwa Mpete aliwahimiza madiwani wote kuwa mabalozi wa utalii kwa kuhamasisha wananchi katika maeneo yao kutenga muda wa kutembelea vivutio vya asili vilivyopo nchini. Alisema kwamba ziara kama hizo zinatoa fursa si tu ya kujifunza, bali pia kupumzisha akili na kusaidia kukuza sekta ya utalii kwa kuongeza idadi ya wageni wa ndani kwenye hifadhi zetu.
“Sisi kama madiwani tuna kazi sasa ya kwenda kuhamasisha wananchi kwenye kata zetu kufanya utalii wa ndani ,Kwa kufanya hivi, tutachangia mapato ya serikali " alisema Mheshimiwa Mpete.
Diwani wa Viti Maalum, Mheshimiwa Angela Mwangeni, alitoa pongezi na shukrani kwa Mwenyekiti wa Halmashauri kwa kuona umuhimu wa madiwani kushiriki katika utalii wa ndani. Alisema hatua hiyo ni mfano bora wa kuonyesha njia kwa wananchi na kuchochea ari ya kutembelea vivutio vya kitalii.
“Ninampongeza sana. Mwenyekiti kwa kutambua kuwa sisi kama viongozi tunaweza kutoka na kufanya utalii,nimekuwa Diwani kwa muda mrefu mrefu jambo kama hili halijawaji kutokea .Tumeona na kujufunza wageni ni wengi kutoka Kenya na nchi nyingine ni jukumu letu sasa kuwaelimisha wananchi kuhusu utalii wa ndani. Ziara hii imetufungua macho kuhusu thamani ya rasilimali tulizonazo,” alisema Mheshimiwa Mwangeni.
Wakiwa katika hifadhi ya Tarangire walipata fursa ya kujionea uzuri wa Hifadhi ya Tarangire, maarufu kwa wanyama wakubwa kama tembo ,twiga na simba, pamoja na miti yake ya kipekee ya mibuyu.
Ziara hiyo ni kielelezo cha umuhimu wa utalii wa ndani katika kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Ofisi yetu inapatikana barabara ya Njombe-Songea mtaa wa Mjimwema.
Sanduku la Posta: S.L.P 577
Simu ya Mezani: 026-2968833
Simu ya Mkononi: 026-2968833
Barua Pepe: td@njombetc.go.tz
Haki Miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Njombe