Waziri wa Nyumba na Maendeleo ya makazi Angelina Mabula ameagiza kuwa mashamba yaliyokuwa yamemilikishwa kwa Chama Cha Ushirika Mkoa wa Njombe (NJORECU) na baadaye Wananchi kuyatumia mashamba hayo kuyaendeleza kwa muda mrefu, kufanyiwa upimaji upya na kukaa chini na pande zote mbili wakiwemo Wananchi wa Kijiji cha Ihanga na NJORECU ili kuona namna bora ya ugawaji wa maeneo hayo ambayo yatakuwa yamepimwa upya.
Awali akiwasilisha taarifa ya Kamati maalumu iliyoundwa kwa lengo la kutatua migogoro ya muingiliano wa kimatumizi katika Vijiji 975 Tanzania nzima Kijiji cha Ihanga Halmashauri ya Mji Njombe kikiwa ni miongoni mwa Vijiji vilivyofikiwa; Upendo Muguzi Mpima Ardhi kutoka Wizara ya Nyumba na Maendeleo ya Makazi alisema kuwa, Kamati hiyo ilibaini kuwa NJORECU walimilikishwa maeneo hayo tangu mwaka 1993 kwa barua ya Toleo na tangu kufanyika kwa umilikishwaji huo maeneo hayo hayakuwahi kuendelezwa na Serikali ya Kijiji kuchukua uamuzi wa kuwagawia Wananchi.
Wakichangia katika nyakati tofauti tofauti baadhi ya Wajumbe wa Kamati hiyo na Viongozi kutoka Halmashauri ya Mji Njombe akiwemo Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri Filoteus Mligo, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Njombe Ester Gama amesema kuwa ni vyema eneo hilo ambalo limebainika kuwa na ekari 244 tofauti na nyaraka za umiliki zinazoonyesha kuwa na ekari 392 sawa na ekari 968.5 kumilikishwa kwa Wananchi wa Kijiji hicho kwani kwa muda mrefu NJORECU walilitelekeza bila kuliendeleza na hivyo kuwapasa kuomba eneo lingine kama nia yao inaendelea kuwepo.
Ziara hii ni mwendelezo wa ziara ya Mawaziri wa Wizara za Kisekta kutembelea Nchi nzima na kutatua migogoro ambapo leo wamefika katika Mkoa wa Njombe ukiwa ni Mkoa wa 22 tangu kuanza kwa ziara hiyo.Mawaziri wanaoshiriki ni kutoka katika wizara ya Nyumba na Maendeleo ya makazi Ikiwakilishwa na Waziri wa Wizara hiyo Angelina Mabula, Wizara ya Kilimo na Umwagiliaji ikiwakilishwa na Naibu Waziri Antony Mavunde, Wizara ya Mifugo na Uvuvi ikiwakilishwa na Naibu Waziri Abdallah Ulega , Wizara ya Maliasili na Utalii ikiwakilishwa na Naibu Waziri Mary Masanja, Ofisi ya Rais TAMISEMI ikiwakilishwa na Naibu Waziri David Silinde , Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira ikiwakilishwa na Naibu Waziri Khamis Hamza Chillo na Wizara ya Maji ikiwakilishwa na Naibu Waziri Mhandisi MaryPrisca Mahundi.
Ofisi yetu inapatikana barabara ya Njombe-Songea mtaa wa Mjimwema.
Sanduku la Posta: S.L.P 577
Simu ya Mezani: 026-2968833
Simu ya Mkononi: 026-2968833
Barua Pepe: td@njombetc.go.tz
Haki Miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Njombe