Halmashauri ya Mji Njombe kupitia Idara ya Utumishi na Utawala imetoa mafunzo ya siku moja kwa watumishi waliopata ajira kwa mwaka 2022/2023 katika Halmashauri, lengo la mafunzo hayo ikiwa ni kupunguza makosa katika utendaji kazi wao wa kila siku, kujua haki na wajibu wao ili kuongeza nidhamu na uwajibikaji katika kazi.
Akizungumza katika mafunzo hayo Mkuu wa Idara ya Utumishi na Utawala Ester Gama amesema kuwa mafunzo hayo ni hatua ya awali kwa kila mtumishi wa umma kwani yapo makosa yanayokuwa yakifanywa na Watumishi kutokana na kutokujua na ndio maana wameona ni vyema kufanya mafunzo hayo ambapo amesema kuwa idara yake imejipanga kuendelea kutoa mafunzo ya mara kwa mara na ufuatiliaji ilikuweza kukumbusha na kutoa elimu zaidi za wajibu wa kila mtumishi wa umma.
Akifungua mafunzo hayo Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Njombe Kuluthum Sadick amewataka Watumishi hao kuhakikisha kuwa wanatumia nafasi waliyoipata kufanya kazi kwa bidii na ubunifu bila kujali mazingira ya kazi yanayowazunguka.
“Nimefurahi kwanza wengi wenu hapa ni vijana nafasi uliyopewa uifanyie kazi kwani wapo wengi ambao mpaka sasa hawajapata ajira na wanatamani kupata kazi kama hiyo uliyonayo. Usiwe mtu wa kukimbia kimbia kila mtu amekuja mwenyewe na kila mtu ataondoka mwenyewe yasikilize yaliyo mazuri ambayo hayastahili yaache.”Alisema Mkurugenzi.
Katika hatua nyingine Kuluthum amewataka Watumishi hao hususani katika Idara ya Afya kuhakikisha kuwa wanakuwa na lugha nzuri kwa Wagonjwa na kutoa huduma kwa upendo ili kuwa mfano wa kuigwa kwa jamii lakini pia hata kwa wale ambao watakaowakuta ili kutengeneza taswira zao na kuweza kuwatofautisha kati ya mtu mmoja na mwingine.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Halmashauri Daktari Yesaya Mwasubila amewataka Watumishi hao kufanya usimamizi wa mapato na matumizi ya dawa na kuwa na kumbukumbu sahihi juu ya matumizi bora ya dawa na mapato yatokanayo kwenye vituo hivyo.
Ikimbukwe kuwa katika kipindi cha kuanzia Julai mwaka 2022 Halmashauri ya Mji Njombe imepokea jumla ya watumishi 56 katika mchanganuo ufuatao Idara ya Afya Watumishi 35, Elimu Sekondari Watumishi 11, Elimu Msingi Watumishi 4 na Utawala Watumishi 6.
Ofisi yetu inapatikana barabara ya Njombe-Songea mtaa wa Mjimwema.
Sanduku la Posta: S.L.P 577
Simu ya Mezani: 026-2968833
Simu ya Mkononi: 026-2968833
Barua Pepe: td@njombetc.go.tz
Haki Miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Njombe