Mbunge wa jimbo la Njombe Mjini Mheshimiwa Deo Mwanyika amekabidhi mifuko ya saruji 2850 yenye thamani ya shilingi milioni 31.9 katika kata mbalimbali za Halmashauri ya Mji Njombe.
Akizungumza katika makabidhiano hayo Mwanyika amesema kuwa katika ziara zake ambazo alizokuwa akizifanya kwenye vijiji na mitaa changamoto kubwa na kilio kikubwa cha Wananchi ilikuwa ni maombi ya saruji kwa ajili ya kusaidia utekelezaji wa miradi kwenye maeneo mbalimbali
“Katika ziara zangu zote nimezifanya hakuna risala ambayo haikuwa na mahitaji ya saruji. Wananchi Wananchangia, Halmashauri inachangia, Serikali Kuu inachangia na Mbunge anachangia. Hakuna eneo nililopita ambalo hawakutamka mahitaji ya saruji. Na mimi kwa kuliona hilo nikaamua kununua kwa pamoja saruji ili kuweza kupunguza changamoto hiyo.Ni kweli kuwa katika kila Kata kuna shughuli za ujenzi zinafanyika na takwa kubwa limekuwa ni mahitaji ya saruji.”Alisema Mwanyika.
Aliendelea kusema”Niliona ni vizuri kutatua tatizo hilo hatuwezi kulimaliza kwani ujenzi ni shughuli endelevu. Msimamo wangu mimi ni kuwa hatutoi mifuko hii ya saruji ili ikakae bila kufanya kazi. Tunamifuko 2850 ambapo kati ya hiyo mifuko 2125 tumetoa kupitia fedha za mfuko wa jimbo na mifuko 725 ikiwa ni mchango wangu binafsi.Katika kila Kijiji kitapatiwa mifuko 50 ya Saruji na Kata zitapatiwa mifuko 150 ya Saruji. Nipende kuwasihi na kuwaonya kuwa ninyi ndio wasimamizi wakuu wa shughuli za maendeleo kwa Wananchi tukafanye kazi kwa uadilifu na usimamizi wa karibu ili ikatumike kwa kadri ya makusudio”Alisema Mbunge
Wakitoa shukrani zao baadhi ya Watendaji akiwemo Neema Mtama Afisa Mtendaji Kijiji cha Lwangu na Christina Mgimba Afisa Mtendaji Kata ya Mjimwema wamesema kuwa Wanamshukuru sana Mheshimiwa Mbunge kwa msaada huo kwani wanaamini kuwa itasaidia kufikisha miradi hiyo kwenye hatua kubwa lakini pia itawatia moyo Wananchi kuendelea kuchangia miradi ya maendeleo.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Njombe Bi.Kuluthum Sadick amemshukuru Mheshimiwa Mbunge kwa kutekeleza ahadi yake na amesema kuwa kwa hatua ya sasa mifuko hiyo itasaidia sana kwenye kufanikisha miradi hiyo.
Ofisi yetu inapatikana barabara ya Njombe-Songea mtaa wa Mjimwema.
Sanduku la Posta: S.L.P 577
Simu ya Mezani: 026-2968833
Simu ya Mkononi: 026-2968833
Barua Pepe: td@njombetc.go.tz
Haki Miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Njombe