Mkuu wa Mkoa wa Njombe Mheshimiwa Anthony Mtaka, Aprili 26,2024 ameshiriki pamoja na wananchi mkoani Njombe, kupanda miti 1000 aina ya mivengi kwenye bonde la Lunyanywi ikiwa ni siku maadhimisho ya miaka 60 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Akizungumza na wananchi walioshiriki maadhimisho hayo kwenye viwanja vya Halmashauri ya Mji Njombe, Mheshimiwa Mtaka amewakumbusha wananchi wa Njombe umuhimu wa muungano.
"Muungano huu ni fahari yetu hatuna mama mwingine zaidi ya mama Tanzania,ni lazima tutembee tukiona ufahari wa muungano ambao ni kielezo na mfano kwa dunia, muungano wetu ni tunu muungano wetu ni lulu, tufanye kazi tukiamini nchi yetu ni moja ambayo ni Tanzania. "Alisema akinukuu hotuba ya Mhe. Rais aliyoitoa Aprili 25,2024.
Aidha aliwataka wananchi wa Njombe kuhakikisha wanaendelea kuhamasishana kupanda miti haswa miti ya matunda ili kuboresha lishe.
" Wito wangu ningetamani kuona tunahamasika pia kupanda miti ya matunda kwenye familia na maeneo ya shule ili watoto waweze kula matunda kuanzia nyumbani na shuleni wakati wa chakula"
Katika hatua nyingine alikemea vikali vitendo vya uchomaji moto kwenye misitu na mashamba ya miti.
"Ni lazima tukemee tabia hizi za hovyo za visasi na hujuma kwa kuchoma mashamba ya miti, Mkoa wetu ni wa pili kwa upandaji wa miti, msisitizo wangu tujiepushe na vitendo vya kuchoma moto mashamba, moto unakatisha tamaa kwa wawekezaji wapya, kilimo cha miti ni kilimo cha biashara, kinazalisha ajira, ni lazima tuulinde uchumi wa Mkoa wetu tukemee uchomaji wa misitu."
Maadhimisho ya miaka 60 ya Jamhuri ya Muungano Mkoa wa Njombe yamefanyika Wilaya ya Njombe na kuhudhuria na wananchi pamoja wataalamu kutoka ofisi ya Mkuu wa Mkoa Njombe,Halmashauri ya Wilaya ya Njombe, Njombe Mji na Makambako Mji pamoja na viongozi wengine wa kisiasa.
Kaulimbiu ya maadhimisho ya siku ya muungano inasema "Tumeshikamana na Tumeimarika kwa Maendeleo ya Taifa letu."
Ofisi yetu inapatikana barabara ya Njombe-Songea mtaa wa Mjimwema.
Sanduku la Posta: S.L.P 577
Simu ya Mezani: 026-2968833
Simu ya Mkononi: 026-2968833
Barua Pepe: td@njombetc.go.tz
Haki Miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Njombe