Halmashauri ya Mji Njombe imetoa mikopo yenye thamani ya shilingi milioni 368,550,000/= kwa vikundi 34 vya wanawake vijana na walemavu katika kipindi cha robo ya tatu ya mwaka 2021/2022 huku shughuli kubwa za wanavikundi hao zikiwa ni kilimo, ufugaji ufundi ushonaji, kuosha magari, uokaji na biashara za duka.
Akiwasilisha taarifa fupi ya utoaji wa mikopo hiyo Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii Halmashauri ya Mji Njombe Bi. Enembora Lema amesema kuwa vikundi 34 viliweza kutembelewa na kukidhi vigezo, ambapo vikundi 10 vya wanawake vimepatiwa mkopo wa shilingi milioni 136, vikundi 18 vijana mkopo wa shilingi milioni 208 laki 7 na 6 watu wenye ulemavu kiasi cha shilingi milioni 23 na laki 8.
“Niwapongeze sana wanavikundi wa Njombe. Asilimia kubwa ni wakopaji na warejeshaji. Kuna maeneo mengi watu wanahangaika kwenye urejeshaji wa mikopo hii ila kwa Njombe mmekuwa warejeshaji wazuri. Niwaombe sasa mkasimamie miradi ili iwe endelevu.”Alisema Afisa Maendeleo ya Jamii.
Akizungumza katika hafla ya utoaji wa mikopo hiyo Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Njombe Mhe. Erasto Mpete amesema kuwa hali ya utoaji mikopo katika Halmashauri imeendelea kuimarika mwaka hadi mwaka na hii inatokana na namna Halmashauri ilivyojipanga katika zoezi zima la uchangiaji wa mapato na namna elimu ya ulipaji kodi ilivyowafikia Wananchi Mjini Njombe.
“Niwaombe sana mikopo mliyopatiwa ikatumike kwa matumizi yaliyoombewa kwani kukiuka vigezo hivyo mnakwenda kinyume na sheria na kanuni za utoaji mikopo kwani kikundi kitakuwa kimepoteza sifa ya ukopaji. Mikopo hii inatakiwa pia iwasaidie na wengine hivyo niwaombe Idara ya Maendeleo ya Jamii kufuatilia mikopo hii ili mfuko uwe endelevu” Alisema Mpete.
Baadhi ya Taasisi zilizoshiriki kutoa elimu mbalimbali kwa wanavikundi hao zimefurahishwa na muitikio wa Wananchi kuchangamkia fursa hiyo na kuwataka Wananchi wanaolalamika kuacha na badala yake kutumia fursa ya mikopo ya Halmashauri kupata mitaji ya kuendeshea shughuli za ujasiriamali na kiuchumi.
Mwakilishi kutoka Taasisi ya Kupambana na rushwa TAKUKURU Daniel Mntambo amesema kuwa lengo la wao kushiriki katika hafla hiyo ya utoaji mikopo ni kuhakikisha kuwa hakuna viashiria vyovyote vya rushwa vinavyokuwepo katika zoezi zima la utoaji mikopo.Aidha Taasisi nyingine zilizoweza kushiriki na kutoa elimu kwa wanavikundi hao ni pamoja na jeshi la polisi kitengo cha usalama barabarani, ofisi ya Hakimu Mkazi Wilaya ya Njombe na Ofisi ya kuzuia na kupambana na rushwa TAKUKURU.
Baadhi ya Wawakilishi kutoka katika makundi mbalimbali ambao ndio wanufaika wa mikopo hiyo likiwemo kundi la Walemavu Angela Kilasi,Herman Sanga mwakilishi wa Vijana na Grace Mbwilo kwa upande wa Wanawake amesema kuwa anaipongeza Serikali kwa kuweza kufikia makundi mbalimbali ya wahitaji.
“Naipongeza Serikali kwa kuweza kutoa mikopo mpaka kwa sisi Walemavu.Walemavu wengi wapo ila wamejificha hawatoki kwa sababu hawana vitu vya kuwatoa ndani. Ila kupitia sisi tunaopata mikopo naamini wengi watakwenda kutoka na tutakwenda kuwa mabalozi kuwa mikopo kwa walemavu inawezekana.”Alisema Angela Kilasi mwakilishi wa Walemavu
Halmashauri ya Mji Njombe imeendelea kutekeleza maagizo ya Serikali na kutekelza sheria ya fedha ya Serikali za Mitaa kifungu cha 37(A) ambayo inazitaka Halmashauri kutenga asilimia kumi ya mapato yake ya ndani kwa ajili ya kusaidia vikundi vya Wanawake,Vijana na Walemavu kwa kutoa mikopo isiyo na riba.
Ofisi yetu inapatikana barabara ya Njombe-Songea mtaa wa Mjimwema.
Sanduku la Posta: S.L.P 577
Simu ya Mezani: 026-2968833
Simu ya Mkononi: 026-2968833
Barua Pepe: td@njombetc.go.tz
Haki Miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Njombe