Katika kuboresha mazingira ya upatikanaji wa elimu bora kwa wanafunzi na uwepo wa mazingira rafiki ya utoaji wa huduma bora za afya, Halmashauri ya Mji Njombe kupitia mapato ya ndani Halmashauri imechangia kiasi cha Shilingi Milioni 97 laki 4 kwa ajili ya ununuzi wa samani katika Shule 7 za Sekondari na Zahanati mpya 5.
Akisoma taarifa ya hali ya utekelezaji wa mpango wa utengenezaji madawati kwa Shule za Sekondari zoezi lililoanza kufanyika mwezi Desemba 2020 mpaka sasa, Afisa Elimu Sekondari Procheus Nguli amesema kuwa licha ya Halmashauri kuendelea kutekeleza miradi mingine mpango wa kutengeneza madawati 775 ulifuatia uwepo wa Shule mpya ya Utalingolo na Kibena zilizoanza rasmi mwaka huu 2021 jambo lililopelekea ongezeko la uhitaji wa samani na kukidhi mahitaji ya samani katika shule nyingine za Sekondari zilizokuwa na uhitaji.
“Tulifanikiwa kutengeneza madawati 320 ambayo yameanza kutumika katika Shule mpya mbili ambazo ni Shule ya Sekondari Utalingolo na Shule ya Sekondari Kibena.Sekondari nyingine zitakazopatiwa samani hizo ni Shule ya Sekondari Matola madawati 160,Uliwa 105,Mgola 90,Kifanya 80 na Viziwi madawati 20.”Alisema Nguli
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Halmashauri Dkt. Yesaya Mwasubila amesema kuwa Halmashauri imeweza kununua meza 35, viti 65, makabati 10,na rafu 10 na viti vya aluminium 15 vifaa vilivyogharimu kiasi cha shilingi milioni 35 laki 4.
Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Njombe Romanus Mayemba amesema kuwa zoezi la utoaji huduma kwa Wananchi ni zoezi endelevu na amewaomba wote waliokabidhiwa samani hizo kwa upande wa afya na elimu kuhakikisha utunzaji wake ili ziweze kuwa na manufaa hata kwa baadaye.
“Tunapotoa huduma ni vyema kutambua kuwa kuna fedha ya Serikali na michango ya Wananchi iliyotumika kununua vifaa hivyo.Halmashauri itaendelea kutoa huduma hizi kadri ambavyo Mwenyezi Mungu atakuwa amejalia lakini pia niwasihi Wananchi kuendelea kuchangia mapato ya Halmashauri na kusimamia mapato kwenye maeneo yao na kama kunaupotevu wowote tupeane taarifa kwani mapato haya ndio yanasaidia kupata huduma kama hizi na hatimaye kuleta maendeleo kwenye maeneo yetu”Alisema Mwenyekiti wa Halmashauri.
Akipokea samani hizo kwa niaba ya Wakuu wa Shule zitakazonufaika,Mkuu wa Shule ya Sekondari Uliwa Robert Emmanuel amesema kuwa anaipongeza Halmashauri kwa jitihada kubwa ambayo imekuwa ikionesha katika kutekelza miradi yake kupitia mapato ya ndani na ameahidi kuendelea kusimamia ufaulu katika shule kwani Halmashauri imekua na msaada mkubwa kwao na fadhila pekee ni kuhakikisha Halmashauri inakuwa na kiwango kikubwa cha ufaulu katika ngazi za kitaifa.
Ofisi yetu inapatikana barabara ya Njombe-Songea mtaa wa Mjimwema.
Sanduku la Posta: S.L.P 577
Simu ya Mezani: 026-2968833
Simu ya Mkononi: 026-2968833
Barua Pepe: td@njombetc.go.tz
Haki Miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Njombe