Zikiwa zimebaki siku 5 kwa Halmashauri ya Mji Njombe kuupokea Mwenge wa Uhuru, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Bi. Kuruthum Sadick Juni 12,2024 amefanya ziara pamoja na menejimeti ya Halmashauri iliyokuwa na lengo la kuangalia njia na hatua za maandalizi ya mapokezi ya Mwenge kwenye miradi ya maendeleo.
Halmashauri ya Mji Njombe inatarajia kupokea Mwenge wa Uhuru Tarehe 17 Juni, 2024 kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa Katika kijiji cha Boimanda kilichopo kata ya Matola.
Baada ya shughuli ya mapokezi, Mwenge wa Uhuru utakimbizwa kwenye miradi mbalimbali ya maendeleo iliyopo katika kata 6 ambazo ni, kata ya Matola ambapo utafanyika Uzinduzi wa vyumba 3 na ofisi 1 Shule ya Msingi Boimanda na Uzinduzi wa wimbo wa kikundi cha kwaya unaohamasisha uchaguzi wa Serikali za mitaa mwaka 2024 pamoja nakutoa cheti, kata ya Uwemba utafanyika Ukaguzi wa Msitu wa hifadhi wa asili wa Isililo pamoja na kugawa mizinga 10 kwa kikundi cha wafugaji wa nyuki, kata ya Yakobi utafanyika Ukaguzi wa shamba la parachichi lenye ukubwa wa ekari 200, kata ya Mjimwema utafanyika Uzinduzi wa kituo cha mafuta cha Amoil, kata ya Njombe Mjini utafanyika Ukaguzi wa kikundi cha vijana cha Sungura Njombe (SUNJO) na ukaguzi wa klabu ya kupinga Rushwa katika shule ya Sekondari Mpechi na katika kata ya Ramadhani utafanyika Uzinduzi wa jengo la mama na mtoto katika hospitali ya Mji Njombe (Kibena).
Aidha Mwenge wa Uhuru baada yakukamilisha kutembelea miradi ya maendeleo , utaelekea kwenye mkesha utakaofanyika viwanja vya stendi ya zamani Njombe Mjini.
Wananchi wote mnakaribishwa kuupokea Mwenge wa Uhuru kwenye miradi iliyopo katika maeneo yenu, kukesha na Mwenge wa uhuru na kuukabidhi Mwenge wa Uhuru Halmashauri ya Wilaya ya Makete.
Kauli mbiu ya Mbio za Mwenge wa Uhuru 2024 inasema "Tunza mazingira na shiriki Uchaguzi wa Serikali za mitaa kwa Ujenzi wa Taifa Endelevu".
Ofisi yetu inapatikana barabara ya Njombe-Songea mtaa wa Mjimwema.
Sanduku la Posta: S.L.P 577
Simu ya Mezani: 026-2968833
Simu ya Mkononi: 026-2968833
Barua Pepe: td@njombetc.go.tz
Haki Miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Njombe