Mkurugenzi wa Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe Ofisi ya Rais-TAMISEMI Dr.Ntuli Kapologwe amepongeza kasi ya ujenzi wa vituo vya afya unaofanywa na Halmashauri ya Mji Njombe ambapo mpaka sasa Halmashauri ipo katika hatua za mwisho za kukamilisha vituo viwili vya Afya Makowo na Kifanya kupitia michango ya Wananchi na mapato ya ndani ya Halmashauri hiyo.
Akizungumza wakati wa ziara yake ambapo alipata nafasi ya kutembela Kituo cha afya Kifanya Dkt Ntuli amesema kuwa Halmashauri ya Mji Njombe ni miongoni mwa Halmashauri zilizoweza kufanya vizuri kwenye utekelezaji wa miradi ya afya kupitia mapato ya ndani na ni vyema Halmashauri nyingine kuiga mfano huo.
“Uongozi unaweza kufanya mabadiliko makubwa sana. Menejimenti mnaongea lugha moja hicho ni kitu kizuri sana na ndio maana kwa pamoja mnaweza kutekeleza haya yote. Hayo maono uliyonayo na dhana ya ushirikishwaji na mikakati ni mambo ambayo Wakurugenzi katika maeneo mengine wanatakiwa waige mfano kama huu. Kuna maeneo mengine Wakurugenzi hata kushiriki katika kutekeleza miradi ya afya ni ngumu. Nimefurahi kwani kwa kipindi nilipokuja mathalani katika Hospitali ya Kibena na leo nilivyoiona mabadiliko ni makubwa sana niwapongeze sana.Lakini kubwa kwenye vituo vya afya mmepiga hatua kubwa”Alisema Dr. Ntuli
Dr. Ntuli amesema kuwa ni vyema katika Vituo vya Afya kuweka uhifadhi wa mazingira kwa kupanda miti ya matunda kwenye bustani zinazozunguka maeneo ya Hospitali
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Njombe Illuminatha Mwenda amesema kuwa Halmashauri imejiwekea utaratibu wa kufanya vikao viwili kila wiki ambapo menejimenti hujadili taarifa za mapato katika vyanzo vyote zikiwemo hospitali na vituo vya afya jambo ambalo Wakuu wa Idara hushiriki na kutoa mawazo juu ya jitihada za ukusanyaji mapato.
“Kwenye makusanyo huwa tunakusanya kwa asilimia mia moja na kuwa na zidio.Hii imepelekea Halmashauri kuweza kupeleka fedha katika miradi ya afya na ndio maana kwa sasa tupo katika kukamilisha vituo viwili vya afya Kifanya na Makowo. Halmashauri kupitia mapato ya ndani zidio la makusanyo kwenye bajeti ya mwaka 2019/2020 kwa kituo afya Kifanya kilipokea milioni 290 na Makowo 290 milioni. Kuchangia jitihada za wananchi. Hiyo ikiwa ni kwenye zidio la makusanyo.” Alisema Mwenda.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Mji Njombe Dr. Yesaya Mwasubila amesema kuwa changamoto kubwa kwa sasa mara baada ya kukamilika kwa vituo hivyo ni uwepo wa Madakatari na wataalamu wa mionzi ambapo Dr. Ntuli amesema kuwa Serikali imeendelea kulifanyia kazi jambo hilo kwa kuajiri Wataalamu katika Sekta hiyo.
Katika ziara hiyo Dr. Ntuli ameahidi upatikanaji wa vifaa tiba katika Vituo hivyo mara baada ya kukamilika na kuahidi uboreshaji wa kituo cha afya Njombe Mjini na ujenzi wa kituo kipya cha afya Mjimwema huku Halmashauri ikitaraji kuanzisha ujenzi wa kituo kingine kipya katika Kata ya Luponde.
Ofisi yetu inapatikana barabara ya Njombe-Songea mtaa wa Mjimwema.
Sanduku la Posta: S.L.P 577
Simu ya Mezani: 026-2968833
Simu ya Mkononi: 026-2968833
Barua Pepe: td@njombetc.go.tz
Haki Miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Njombe