Julai 30, 2025 Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Njombe, Bi. Kuruthum Sadick, amezindua rasmi kliniki ya ardhi katika Kijiji cha Kifanya, ikiwa ni hatua ya kuwasogezea wananchi huduma karibu na maeneo yao ya makazi.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo , Bi. Sadick amewataka wananchi wa Kifanya na vijiji jirani kuitumia ipasavyo fursa hiyo muhimu, ili kupata umiliki halali wa ardhi kwa kufuata taratibu na sheria zilizowekwa.
"Ni wajibu wetu kuhakikisha kila mwananchi anamiliki ardhi kwa mujibu wa sheria. Kliniki hii ni nafasi ya kipekee kwa wananchi kupata msaada wa kitaalamu kuhusu masuala ya ardhi, bila kusafiri umbali mrefu kufuata huduma hizo," alisema Bi. Sadick.
Kwa upande wake, Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Ardhi Halmashauri ya Mji Njombe, Emmanuel Luhamba, alisema huduma ya kliniki hiyo imeanza rasmi leo tarehe 30 Julai na itaendelea kutolewa kulingana na mahitaji na idadi ya wananchi watakaojitokeza.
"Kliniki hii itakuwa endelevu kwa muda ambao utaendana na mwitikio wa wananchi. Tunawahimiza wote wenye changamoto au mahitaji ya usajili wa ardhi kufika kwa wakati ili kupata huduma," alisema Luhamba.
Kliniki ya ardhi inatarajiwa kusaidia kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu haki na wajibu wao katika umiliki wa ardhi, pamoja na kuondoa migogoro ya ardhi inayosababishwa na kutokuwepo kwa hati miliki halali.
Ofisi yetu inapatikana barabara ya Njombe-Songea mtaa wa Mjimwema.
Sanduku la Posta: S.L.P 577
Simu ya Mezani: 026-2968833
Simu ya Mkononi: 026-2968833
Barua Pepe: td@njombetc.go.tz
Haki Miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Njombe