Njombe, 14 Februari 2025 – Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Mhe. Anthony Mtaka, amewataka Wenyeviti wa Vijiji na Mitaa yote 463 ya mkoa huo kuwa mfano wa maadili mema na kuongoza kwa busara, hekima, na weredi ili kuleta maendeleo endelevu kwa wananchi wao.
Akizungumza katika mkutano uliofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Mhe. Mtaka alisisitiza kuwa uongozi ni dhamana inayohitaji uadilifu na uwajibikaji. Alieleza kuwa mwenyekiti wa kijiji au mtaa anapaswa kuwa kielelezo cha nidhamu, haki, na maamuzi sahihi yanayolenga kuimarisha ustawi wa jamii. Aliwataka viongozi hao kuhakikisha wanazingatia misingi ya utawala bora kwa kushirikiana na wananchi katika kutatua changamoto zao.
"Uongozi unabeba sifa ya busara, hekima na weredi. Mwenyekiti anapaswa kuwa mfano wa maadili mema na mwelekeo sahihi kwa wananchi wake," alisema Mhe. Mtaka. Aliongeza kuwa viongozi wasiozingatia maadili wanapoteza imani ya wananchi na kushindwa kutimiza wajibu wao ipasavyo. Mkutano huo ulihudhuriwa na Wenyeviti wa Vijiji na Mitaa kutoka maeneo mbalimbali ya Njombe, ambapo walipata nafasi ya kujadili changamoto na mikakati ya kuboresha utendaji wao katika jamii.
Ofisi yetu inapatikana barabara ya Njombe-Songea mtaa wa Mjimwema.
Sanduku la Posta: S.L.P 577
Simu ya Mezani: 026-2968833
Simu ya Mkononi: 026-2968833
Barua Pepe: td@njombetc.go.tz
Haki Miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Njombe