Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Mhe. Anthony Mtaka, amewataka Wenyeviti wa Vijiji na Mitaa yote 463 ya mkoa huo kutambua majukumu yao kama viongozi wa maendeleo na ustawi wa wananchi, badala ya kuwa mapambo katika jamii.
Akizungumza na Wenyeviti hao, Mhe. Mtaka aliwakumbusha kuwa uongozi ni nafasi ya kutatua changamoto na kuleta maendeleo, hivyo hawapaswi kuitumia kwa maslahi binafsi bali kwa manufaa ya jamii nzima.
Alisisitiza kuwa uongozi unahitaji busara, hekima na weredi, huku Mwenyekiti akitakiwa kuwa mfano wa maadili mema kwa wananchi wake. Aidha, alionya kuhusu uuzaji holela wa maeneo ya vijiji na mitaa, akisema kuwa mwenyekiti anayefanya hivyo anageuka kuwa laana badala ya baraka kwa jamii.
Mhe. Mtaka aliwataka Wenyeviti kuwa sehemu ya suluhisho la matatizo ya wananchi na kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa haki na usawa bila upendeleo wala ubaguzi.
Pia, aliwataka kusimamia sheria za vijiji, hususan zinazohusu matumizi ya moto wakati wa usafishaji wa mashamba ili kuepusha madhara kwa jamii. Alikumbusha kuwa Mwenyekiti ni Afisa Usalama wa kijiji, hivyo ana wajibu wa kuhakikisha wananchi wake wanaishi kwa amani na usalama.
Kwa upande wa maendeleo, aliwakumbusha Wenyeviti kutoruhusu miradi ya maendeleo kuharibika, kwani kila mradi una lengo la kuboresha maisha ya wananchi.
Mhe. Mtaka aliwataka viongozi hao kuwa chachu ya mabadiliko chanya kwa kuhakikisha vijiji na mitaa yao yanakuwa sehemu salama, yenye maendeleo na haki kwa kila mwananchi
Ofisi yetu inapatikana barabara ya Njombe-Songea mtaa wa Mjimwema.
Sanduku la Posta: S.L.P 577
Simu ya Mezani: 026-2968833
Simu ya Mkononi: 026-2968833
Barua Pepe: td@njombetc.go.tz
Haki Miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Njombe