Njombe, 14 Februari 2025 – Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Mhe. Anthony Mtaka, amewataka Wenyeviti wa Vijiji na Mitaa yote 463 ya mkoa huo kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu kwa kuhakikisha wanatatua changamoto za wananchi na kusimamia maendeleo bila kuegemea maslahi binafsi.
Akizungumza katika mkutano uliofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Mhe. Mtaka aliwakumbusha viongozi hao kuwa nafasi walizopewa ni dhamana ya kuleta mabadiliko chanya katika jamii wanazoziongoza. Alisisitiza kuwa kiongozi mzuri ni yule anayeweka mbele ustawi wa wananchi na kuhakikisha maendeleo yanafikiwa kwa usawa bila upendeleo.
"Kiongozi ni sehemu ya utatuzi wa changamoto kwa watu lakini pia ni mleta maendeleo. Usitumie nafasi yako kwa maslahi binafsi bali kwa manufaa ya jamii," alisema Mhe. Mtaka.
Aidha, aliwataka viongozi hao kuwa mfano wa uwajibikaji kwa kusimamia rasilimali za vijiji na mitaa yao kwa uaminifu ili kuhakikisha miradi ya maendeleo inawanufaisha wananchi wote. Pia, alisisitiza umuhimu wa ushirikiano baina ya viongozi na wananchi katika kutafuta suluhisho la changamoto zinazoikabili jamii.
Mkutano huo ulihudhuriwa na Wenyeviti wa Vijiji na Mitaa kutoka maeneo mbalimbali ya mkoa wa Njombe, ambao walipata fursa ya kujadili masuala mbalimbali yahusuyo maendeleo na ustawi wa wananchi wao.
Ofisi yetu inapatikana barabara ya Njombe-Songea mtaa wa Mjimwema.
Sanduku la Posta: S.L.P 577
Simu ya Mezani: 026-2968833
Simu ya Mkononi: 026-2968833
Barua Pepe: td@njombetc.go.tz
Haki Miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Njombe