Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mhe. Batilda Burian, Agosti 29,2025 amefunga rasmi mashindano ya Shirikisho la Michezo ya Serikali za Mitaa (SHIMISEMITA) 2025, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhe. Mohamed Mchengerwa.
Mashindano hayo yaliyoanza tarehe 15 Agosti na kumalizika tarehe 29 Agosti 2025, yameshirikisha Halmashauri 154 kati ya 184 zinazotarajiwa, huku yakihusisha zaidi ya watumishi 4,000 waliopambana katika michezo 15 tofauti.
Akizungumza wakati wa kufunga mashindano hayo, Mhe. Burian amewataka watumishi wa umma kuiga mshikamani na mshirikiano uliooneshwa kwenye michezo, hususan kuelekea uchaguzi ujao. “Siku ya uchaguzi siyo siku ya mapumziko, kila mtumishi anatakiwa kuwa mfano wa kuiga kwa kujitokeza kupiga kura kwa ajili ya maendeleo ya taifa letu,” alisema.
Ameeleza kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameonesha dhamira thabiti ya kuimarisha sekta ya michezo nchini kwa kuwekeza kwenye miundombinu, hatua ambayo imewezesha wanamichezo kushiriki mashindano mbalimbali ndani na nje ya nchi.
Aidha amewasilisha maagizo ya Mhe.Mchengerwa ambaye, amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri kuhakikisha wanatenga fedha kwa ajili ya michezo na kuwezesha ushiriki wa Halmashauri zote, na zile zenye changamoto za kifedha kuweza kushiriki michezo michache.Amesisitiza kuwa Halmashauri ambazo hazikufanya vizuri mwaka huu, zijipange mapema na kuendelea na mazoezi ya kila siku ili kujipatia ushindi katika mashindano yajayo.
Vilevile, ameitaka Kamati Tendaji ya SHIMISEMITA kufanya tathmini ya kina ili kuboresha zaidi mashindano yajayo na kuhakikisha yanakuwa bora na yenye ushiriki mpana zaidi.
Katika hafla hiyo Mhe.Batilda ametoa tuzo na zawadi kwa washindi mbalimbali katika mashindano hayo ambapo mshindi wa Jumla ni Halmashauri ya Jiji la Dodoma
Ofisi yetu inapatikana barabara ya Njombe-Songea mtaa wa Mjimwema.
Sanduku la Posta: S.L.P 577
Simu ya Mezani: 026-2968833
Simu ya Mkononi: 026-2968833
Barua Pepe: td@njombetc.go.tz
Haki Miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Njombe