Aprili 28, 2025 Mkuu wa Wilaya ya Njombe, Mheshimiwa Juma Sweda, ametoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi kuwapeleka watoto wao katika vituo vya kutolea huduma za afya ili kupata dozi ya pili ya chanjo ya sindano ya Polio (IPV2).
Akizungumza katika kikao cha Kamati ya Afya ya Msingi kilichowakutanisha viongozi wa Halmashauri ya Mji wa Njombe na Wilaya ya Njombe, Mhe. Sweda alisisitiza kuwa kila kituo cha afya kinapaswa kuendelea kutoa elimu kwa kina mama na jamii kwa ujumla kuhusu umuhimu wa chanjo hiyo.
"Lengo letu ni kuimarisha kinga dhidi ya ugonjwa wa kupooza kwa watoto. Hii si chanjo mpya, bali ni kuongeza dozi ya pili ili kuimarisha zaidi kinga ya mwili kwa watoto wetu ambao ni taifa la kesho," alisema Mhe. Sweda.
Aidha, Mhe. Sweda amehimiza kuwa uhamasishaji na uelimishaji jamii kuhusu chanjo hii uwe endelevu, kwa kutumia mbinu mbalimbali ikiwemo kutoa elimu vituoni na wakati wa huduma mkoba.
Halmashauri ya Mji wa Njombe inatarajia kuanza rasmi utoaji wa dozi ya pili ya chanjo ya sindano ya Polio kuanzia tarehe 1 Mei 2025. Chanjo hii itatolewa kwa watoto kuanzia umri wa miezi 9 hadi chini ya miaka 5, kupitia vituo vya kutolea huduma za afya na huduma mkoba.
Chanjo ya sindano ya Polio (IPV) imeidhinishwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) na Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba nchini (TMDA), na inatolewa kwa utaratibu wa kawaida katika vituo vyote vya afya.
Ofisi yetu inapatikana barabara ya Njombe-Songea mtaa wa Mjimwema.
Sanduku la Posta: S.L.P 577
Simu ya Mezani: 026-2968833
Simu ya Mkononi: 026-2968833
Barua Pepe: td@njombetc.go.tz
Haki Miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Njombe