Mkuu wa Wilaya ya Njombe, Mhe. Juma Sweda, amewataka Maafisa Maendeleo wa Halmashauri ya Mji Njombe kuhakikisha wanatunza kumbukumbu sahihi za waombaji wa mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na Halmashauri, ili kuepusha malalamiko kutoka kwa wananchi wanaokosa mikopo hiyo.
Mhe. Sweda ametoa agizo hilo Septemba 1, 2025, wakati wa hafla ya kukabidhi hundi za fedha na vitendea kazi kwa wanufaika wa mikopo hiyo. Amesema mikopo hiyo hutolewa kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kutokana na mapato ya ndani ya Halmashauri, hivyo ni lazima kuzingatia uwazi na uwajibikaji katika usimamizi wake.
“Ni muhimu kutunza kumbukumbu za waombaji wa mikopo, kwani hatua hii itasaidia kupunguza migogoro ambayo mara nyingi imekuwa ikiwalenga Maafisa Maendeleo na kudaiwa kupendelea. Ili kuepuka changamoto hiyo, ni vyema kuwe na kumbukumbu sahihi za waliowahi kuomba lakini hawakufanikiwa, ili katika awamu zinazofuata waweze kupewa kipaumbele,” alisema Mhe. Sweda.
Kwa upande wake, Afisa Maendeleo wa Halmashauri ya Mji Njombe, Bi. Enembora Lema, alisema kuwa kupitia tathmini iliyofanywa kuanzia ngazi ya Kata hadi Wilaya, jumla ya vikundi 94 vilikidhi vigezo vya kupata mikopo. Vikundi 34 vimepatiwa mkopo wenye thamani ya shilingi 1,518,196,000/= ambapo, vikundi 39 vya wanawake vimepatiwa mikopo yenye thamani ya shilingi 637,540,000/=,vikundi 39 vya vijana vimepatiwa mikopo yenye thamani ya shilingi 697,215,000/=na vikundi 16 vya watu wenye ulemavu vimepatiwa mikopo yenye thamani ya shilingi 183,441,000/=
Mikopo hii ya asilimia 10 ya mapato ya ndani ya Halmashauri hutolewa kila robo mwaka kwa mujibu wa sheria, ikiwa na lengo la kuwawezesha wananchi kiuchumi.
Ofisi yetu inapatikana barabara ya Njombe-Songea mtaa wa Mjimwema.
Sanduku la Posta: S.L.P 577
Simu ya Mezani: 026-2968833
Simu ya Mkononi: 026-2968833
Barua Pepe: td@njombetc.go.tz
Haki Miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Njombe