Ziara ya wajumbe wa Kamati ya fedha Halmashauri ya Mji Njombe ikiongozwa na Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri Erasto Mpete ambapo walitembelea na kukagua miradi inayotekelezwa katika Halmashauri ambapo chanzo cha fedha za miradi hiyo ikiwa ni Mpango wa mapambano dhidi ya UVIKO, nguvu za Wananchi na mapato ya ndani ya Halmashauri.
Akizungumza katika ziara hiyo Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri Erasro Mpete amesema kuwa anaishukuru Serikali kwa kuipatia Halmashauri kiasi cha Shilingi milioni mia saba arobaini kufanikisha ujenzi wa vyumba 37 vya madarasa katika Shule 12 za Sekondari.
Wakisoma taarifa za utekelezaji wa miradi hiyo mara baada ya kutembelewa na Wajumbe wa Kamati hiyo Mkuu wa Shule ya Sekondari Matola Gidion Massawe na Mkuu wa Shule ya Anne Makinda Veronica Mlozi ambapo shule zao zinatekeleza ujenzi wa miradi ya madarasa kupitia fedha za UVIKO wamesema kuwa changamoto kuu iliyosababisha ucheleweshaji wa miradi hiyo imekuwa ni Uhaba wa Saruji.
Nao baadhi ya Wajumbe wa Kamati hiyo wakiwemo Ultrick Msemwa Diwani wa Kata ya Luponde, Honolatus Mgaya Diwani wa Kata ya Makowo na Filoteus Mligo Diwani wa Kata ya Lugenge wametaka miradi hiyo isimamiwe kikamilifu ili iweze kukamilika kwa wakati lakini pia kuwa na ubora uliokusudiwa.
“Madarasa yaliyojengwa yatasaidia sana kutatua upungufu wa vyumba vya madarasa tuliokuwa nao. .Januari tunatarajia kupokea wanafunzi wapya wa kidato cha kwanza na kwa taarifa ambapo tumezipata katika shule tulizopita inaonyesha kuwa hatutakuwa na upungufu wa madarasa.Pia kwa hatua hii Wananchi wamepunguziwa mzigo wa kuchangia.Tunaipongeza Serikali kwa hatua hii.Alisema Mheshimiwa Msemwa Diwani wa Kata ya Luponde.
Katika shule ya Sekondari Yakobi, Shule inayotekeleza ujenzi wa vyumba 06 vya madarasa kwa ajili ya kidato cha tano, na ujenzi wa bwalo la Wanafunzi ambapo Shule hiyo imeweza kuchangia zaidi ya shilingi milioni 15 ikiwa ni fedha za Elimu ya Kujitegemea(EK). Mkuu wa Shule ya Yakobi Editha John amesema fedha za EK zimekuwa na msaada mkubwa kwani Wazazi na Uongozi wa Shule wamekuwa na makubaliano kuchangia mawe na na nyaya za umeme kwa mwanafunzi yeyote atakayesababisha utovu wa nidhamu shuleni hapo.
“Uongozi wa Shule na Wazazi tumekubaliana na hata kwenye fomu za kujiunga tumesema kuwa kwa mwanafunzi ambaye atafanya utovu wa nidhamu shuleni,Mzazi atawajibika kulipa lori moja la mawe na nyaya za umeme bando moja jambo ambalo kwa kiasi kikubwa limesaidia kufanikisha ujenzi wa miradi hiyo.Mfano tumepata tripu zaidi ya 45 za mawe kupitia mfumo huo”Alisema Mkuu wa Shule hiyo
“Huu ni ubunifu wa hali ya juu. Nikupongeze Mkuu wa Shule kwa ubunifu huu na nafikiri kuwa tunaweza kutumia mfumo huu kwa shule nyingine ndani ya Halmashauri.”Alisema Diwani wa Kata ya Lugenge Filoteus Mligo
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Njombe Thadei Luoga amesema kuwa atahakikisha kuwa Walezi wa Kata ambao ni Wakuu wa Idara na Vitengo vya Halmashauri wanaendelea kuisimamia miradi hiyo kwa ukaribu zaidi ili kuhakikisha kuwa miradi hiyo inakamilika kwa wakati na kwa ubora uliokusudiwa.
Ofisi yetu inapatikana barabara ya Njombe-Songea mtaa wa Mjimwema.
Sanduku la Posta: S.L.P 577
Simu ya Mezani: 026-2968833
Simu ya Mkononi: 026-2968833
Barua Pepe: td@njombetc.go.tz
Haki Miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Njombe