Ni ziara ya Naibu waziri TAMISEMI Ndg. Joseph Kandege katika kusimamia kwa ukaribu ukamilishaji wa ujenzi wa stendi mpya ya mabasi Njombe, ikiwa ni jitihada za kuhakikisha agizo la Mheshimiwa Rais alilolitoa katika Ziara yake Mkoani Njombe la kukamilisha ujenzi wa stendi linatekelezwa kufikia tarehe 10 Mei.
Akizungumza mara baada ya kutembelea katika kila hatua ya mradi na kujiridhisha na shughuli za ujenzi zinazoendelea, Kandege alisema kuwa ifikapo tarehe 10 Mei stendi hiyo ianze kutumika kwani kwa hatua iliyofikia sasa haoni sababu zitakazozuia kuendelea kutumilika kwa stendi hiyo.
“Siamini kwamba kwa hatua hii ambayo stendi imefikia itazuia stendi kutumika. Hakuna namna ambavyo tunaweza kujadili agizo la Mheshimiwa Rais. Tuliomba siku 20 akatuongezea siku 10. Ifikapo tarehe 10 Mei naomba stendi ianze kutumika.”Kandege Alisema.
Aliendelea kusema
“Kwa kazi ambazo zimefanyika nawapongeza sana kwa kuonyesha ushirikiano mkubwa. Nilikuja kutizama kabla hatujafika hatua kubwa kama hii na niliamini kwa ushirikiano inawezekana. Naomba tuendelee kuthibitisha kuikamisha stendi kama ambavyo Mheshimiwa Rais aliagiza. Ni vizuri mkaanza kuwatangazia wenye vyombo vya usafiri kuhusu matumizi rasmi ya stendi hii. Wanachi wa Njombe waliisubiria stendi hii kwa muda mrefu sana.”
Ruth Msafiri ni Mkuu wa Wilaya ya Njombe ambaye yeye alisema kuwa anamshukuru Mheshimiwa Rais kwani kupitia maelekezo yake yamefanikisha stendi kufikia hatua ilipo na kuanza kutumika mapema zaidi.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Njombe Illuminatha Mwenda ameishukuru Serikali kwa kuwapatia fedha za utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa stendi ya kisasa Njombe na ameahidi kutekeleza agizo la Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuanza kutumika mara moja ifikapo tarehe 10 Mei.
“Tumeanza kukutana na wadau mbalimbali kwa ajili ya kuweka utaratibu wa matumizi” Alisema Mwenda.
Kwa mujibu wa mratibu wa mradi huo ambaye ni Meneja wa Tarura wa Halmashauri ya Mji Njombe Mhandisi Rais Tembo, alisema kuwa shughuli kubwa ya ujenzi imekamilika na mpaka kufikia tarehe 10 Mei kazi kubwa itakuwa imefanyika na shughuli zitakazosalia hazitakwamisha kuanza kwa matumizi ya stendi hiyo kama ilivyoagizwa.
Kwa wakati huo huo Naibu Waziri Kandege pia alitembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa soko la kisasa Njombe na kuipongeza Halmashauri kwa kuweza kuchagua miradi ya ujenzi wa soko na stendi
“Nina kila sababu ya kuishukuru na kuipongeza Halmashauri ya Njombe TC kwanza katika kuchagua miradi ipi wafanye. Kuna Halmashauri zingine wanachagua miradi ambayo hata hicho kiasi cha fedha zilizotumika ukiambiwa zitarudi unaanza kupata mashaka. Mradi wa Stendi hali kadhalika soko vitakuwa ni vyanzo vya uhakika vya Halmashauri kuingiza mapato.”
Kandege aliongezea kuwa licha ya Halmashauri kunufaika lakini pia kwa kasi ya ujenzi wananchi wanafarijika kwa kazi ambayo inafanyika na watafurahia hali ya kufanya biashara katika mazingira rafiki.
Kandege ametoa rai kwa Halmashauri zingine kupata fursa ya kufika Halmashauri ya Mji Njombe na Kutembelea mradi wa ujenzi wa soko la kisasa na utakapokamilika utakuwa ni miongoni mwa miradi mizuri na yenye ubora wa hali ya juu tofauti na maeneo mengine ambapo miradi kama hii inatekelezwa.
Ujenzi wa soko la kisasa Njombe unatokana na mradi wa ujenzi wa stendi ambapo Halmashauri ililazimika kufanya mapitio ya gharama za ujenzi wa stendi ya mabasi na miundombinu iliyokuwa imependekezwa awali na kufanikiwa kupunguza baadhi ya miundombinu iliyotakiwa kujengwa katika mradi wa ujenzi wa kituo cha mabasi na hivyo kupelekea Halmashauri kuwa na ziada kubwa ya fedha kwa kulinganisha kiasi kilichopangwa kutumika na kile kilichopokelewa na hivyo kupata fedha ambazo ziliwezesha kuanzisha ujenzi wa soko la kisasa.
Ofisi yetu inapatikana barabara ya Njombe-Songea mtaa wa Mjimwema.
Sanduku la Posta: S.L.P 577
Simu ya Mezani: 026-2968833
Simu ya Mkononi: 026-2968833
Barua Pepe: td@njombetc.go.tz
Haki Miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Njombe