Ikiwa zimebaki siku 10 kufikia muda wa Nyongeza uliotolewa na Serikali kukamilisha ujenzi wa vyumba vya madarasa, Naibu waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI David Silinde ameitaka Halmashauri ya Mji Njombe kukamilisha Miradi hiyo ambayo mingi iko katika hatua za mwisho za umaliziaji.
Wito huo umetolewa mara baada ya kukagua ujenzi wa Vyumba viwili vya madarasa katika Shule ya Sekondari Utalingolo na ujenzi wa vyumba vitano vya madarasa katika Shule ya Sekondari Mpechi.
Akizungumza na Wananchi waliofika katika Shule ya Sekondari Luhololo Kata ya Luponde Silinde amesema kuwa Serikali imekua na dhamira ya kuhakikisha kuwa wanafunzi wote waliofaulu kidato cha kwanza wanaingia darasani bila kuwa na awamu ya pili “Second selection”
“Zoezi la ujenzi wa vyumba vya madarasa ni katika Nchi nzima.Lengo lake ni kutatua kero kubwa iliyokuwepo ya upungufu wa madarasa lakini pia kuhakikisha kuwa wale wote wanaofaulu wanaingia darasani kwa mara moja.Na kwa mara ya kwanza Wanafunzi wote waliofaulu kuingia kidato cha kwanza wote wanakwenda darasani mwezi Januari bila ya kuwa na second selection.”
“Serikali pia ipo katika mkakati wa kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za waalimu na ujenzi wa madarasa kwa shule za msingi. Tunajua changamoto ni kubwa lakini kwa kiasi Fulani ujenzi huo utasaidia kutatua changamoto hizo kwa kiasi kikubwa.”Alisema Silinde
Aidha Naibu Waziri amewataka Wazazi na Waalimu kuhakikisha kuwa wanasimamia nidhamu za Wanafunzi na amewaasa Wanafunzi kutoshiriki katika matukio yanayosababisha uharibifu wa miundombinu pamoja na kuchoma moto majengo ambayo yameigharimu Serikali fedha nyingi.
Mbunge wa Jimbo la Njombe Mjini Deo Mwanyika na Diwani wa Kata ya Luponde Ultrick Msemwa na Diwani wa Kata ya Mjimwema Mahenge
Kwa upande wake Katibu Tawala Mkoa wa Njombe Judica Omary amemhakikishia Mheshimiwa Naibu Waziri kuwa atahakikisha wanashirikina na uongozi wa Halmashauri kupiga kambi katika maeneo yenye miradi na kuwahimiza mafundi kufanya kazi usiku na mchana ili miradi hiyo iweze kukamilika kwa wakati kuifikia tarehe ambayo imepangwa na Mkoa ya tarehe 24/12/2021
Ofisi yetu inapatikana barabara ya Njombe-Songea mtaa wa Mjimwema.
Sanduku la Posta: S.L.P 577
Simu ya Mezani: 026-2968833
Simu ya Mkononi: 026-2968833
Barua Pepe: td@njombetc.go.tz
Haki Miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Njombe