Anna Ndawala (57) mkazi wa Kijiji cha Igominyi Kata ya Yakobi ni miongoni mwa mifano mizuri ya namna TASAF III inavyowawezesha wananchi katika kuinua uchumi.
Bi Anna ambaye anapokea kiasi cha shilingi elfu 32,000/= kila baada ya miezi miwili aliingia kwenye mpango mwaka 2015. Mara baada ya kuingia kwenye Mpango Anna alianza shughuli za ufugaji kuku mwanzoni mwa mwaka 2017 na alianza na ufugaji wa kuku 10 wa mayai. Kwa mwaka 2017 Anna alibahatika kuuza vifaranga katika awamu mbili tofauti na kujipatia kipato cha shilingi laki nane.
“Awamu ya kwanza niliuza vifaranga 120, awamu ya pili nikauza vifaranga 56 fedha nilizopata zilinisaidia kufanya shughuli mbalimbali. Nilifanikiwa kununua mahitaji ya shule ya mjukuu wangu, nilinunua mbolea ya kukuzia mahindi na zilinisaidia katika matumizi mbalimbali ya nyumbani. Nilifanikiwa pia kukarabati nyumba yangu na kuweka sakafu kwenye chumba ninacholala pamoja na kusakafia choo.”Alisema Anna
Aidha amefafanua kuwa licha ya kuwepo na changamoto mbalimbali ikiwemo ukosefu wa elimu ya kutosha juu ya mbinu za ufugaji bora na wakisasa kutoka kwa wataalamu wa mifugo na mbinu za kukabiliana na magonjwa lakini bado hajakata tamaa.
Sambamba na hilo Anna ameshauri ni vyema wasimamizi wa wanufaika wa mpango huu ambao ni wanakamati kuhakikisha wanawatembelea wanufaika mara kwa mara ili kukagua shughuli za maendeleo wanazofanya na kujiridhisha kwani wanufaika wengine wamekuwa si wakweli kwani pindi wapokeapo fedha za ruzuku wamekuwa wakizitumia hovyo badala ya kuwekeza katika shughuli za kuwaongezea kipato.
Kwa upande wake Mjukuu wa Mnufaika huyo ambaye anasoma darasa la tano katika shule ya Msingi Igominyi Agape amesema kuwa tangu walipoingia kwenye mpango amekuwa hakosi mahitaji muhimu ya shule kama viatu, madaftari, na ameendelea kufurahia maisha kwani hata katika familia wameweza kuboresha mlo kwa kula Mayai na kitoweo cha Kuku mara kwa mara jambo ambalo halikuwahi kutokea awali.
Kwa sasa Anna ambaye ni mnufaika wa TASAF III anakuku wa kienyeji wapatao 30 wa mayai 200 na kwa siku hukusanya mayai 150 ambayo ni sawasawa na Tray 5 za mayai.
Kufikia mwezi desemba mwaka 2018 Anna amedhamiria kukuza shughuli za ufugaji kuku, kutoka kuku 200 waliopo sasa mpaka kufikia kuku 700 jambo ambalo linamfanya kuishukuru TASAF kwa manufaa aliyoyapata.
Ofisi yetu inapatikana barabara ya Njombe-Songea mtaa wa Mjimwema.
Sanduku la Posta: S.L.P 577
Simu ya Mezani: 026-2968833
Simu ya Mkononi: 026-2968833
Barua Pepe: td@njombetc.go.tz
Haki Miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Njombe