Mkuu wa Wilaya ya Njombe Kissa Gwakisa Kasongwa amesema kuwa bado kuna nafasi kubwa ya kuendelea kuifanya Njombe kuwa safi na kijani muda wote kutokana na kuwa Mkoa wa Njombe haujapata athari kubwa za uchafuzi wa mazingira ukilinganisha na Miji mingine mikubwa ambayo idadi ya watu ni kubwa na uchafuzi wa mazingira upo kwa kiasi kikubwa.
Hayo yamezungumzwa mara baada ya kupokea ugeni kutoka katika Mji wa Miltenberg Nchini Ujerumani ambao ni Mji rafiki na Halmashauri ya Mji Njombe, ikiwa ni hatua ya awali za uanzishaji wa mradi wa kuhakikisha kuwa Njombe inakua safi na kijani, lengo kuu la pili ikiwa ni kuweka nishati mbadala rafiki wa mazingira katika maeneo ya umma kwa kuongeza matumizi ya nishati jua (solar) kwenye maeneo hayo.
“Ninafuraha sana kuwa nanyi leo, Wilaya ya Njombe yenye Halmashauri tatu asilimia kubwa ni ukanda wa miti na misitu. Changamoto kubwa tunayokabiliana nayo hususani katika kipindi hiki cha kiangazi ni uwepo wa moto kichaa ambao unapelekea uharibifu mkubwa wa mazingira na pia kuharibu pato la mtu mmoja mmoja na la Halmashauri kwani yapo mapato yatokanayo na mazao ya misitu yanayochangia kwenye pato la Halmashauri.
Aliendelea kusema sababu kubwa zinazochangia uwepo wa moto kichaa ni pamoja na shughuli za maandalizi ya mashamba wakati wa kilimo na Wananchi kupanda miti bila kufuata ushauri ikiwa ni pamoja na kuweka njia kwa ajili ya kuzuia moto,jambo ambalo Kissa amesema kuwa ni vyema katika program hiyo ikaona namna ya kuweza kutatua changamoto hii ili kuendelea kuilinda misitu yetu na kuwa na utunzaji bora wa mazingira.
Katika hatua nyingine Kissa amefurahishwa na hatua ambayo Mji wa Miltenberg imefanya ya kuhakikisha kuwa Wananchi wanajikwamua kiuchumi kwa uzalishaji wa bidhaa mbalimbali kama vile vinywaji na bidhaa hizo zinapopelekwa sokoni kiasi cha fedha kinachotokana na mauzo hutengwa na kurudishwa kwa wazalishaji hao ikiwa kwa ajili ya kuwawezesha wazalishaji wa bidhaa hizo kuongeza kipato na kuhakikisha kuwa wanakuza biashara zao.
Mji wa Milternberg ni Mji ambao asilia yake inafanana na Wilaya ya Njombe na Wanging’ombe kwa kuwa na hali ya hewa ya baridi kali, upepo na pia zaidi ya asilimia 70 ya Mji huo ukiwa umezungukwa na misitu.
Ofisi yetu inapatikana barabara ya Njombe-Songea mtaa wa Mjimwema.
Sanduku la Posta: S.L.P 577
Simu ya Mezani: 026-2968833
Simu ya Mkononi: 026-2968833
Barua Pepe: td@njombetc.go.tz
Haki Miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Njombe