Mkuu wa Mkoa wa Njombe Antony Mtaka leo amehitisha kikao maalumu kilichowahusisha Watendaji na Viongozi mbalimbali Mkoani Njombe lengo kuu ikiwa kuweka mkakati wa ukamilishaji wa madarasa kabla ya wakati na kuwa na umiliki wa pamoja kwenye ujenzi wa vyumba vya madarasa kazi inayotakiwa kufanyika kwa muda wa siku 75.
Akitoa taarifa za mapokezi ya fedha Katibu Tawala Mkoa wa Njombe Judica Omary amesema kuwa Mkoa wa Njombe umepokea kiasi cha Shilingi Bilioni 1.96 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa 98 katika Mkoa fedha ambazo ni ziada ya bajeti na ambazo zimepokelewa nje ya bajeti ya mwaka 2022/2023.
“Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwani ametuondolea mzigo wa kwenda kuchangisha Wananchi ili kukamisha madarasa haya. Fedha tumeshaletewa na nina amini kuwa kazi haitatushinda kwani hata mwaka jana tuliweza kukamilisha kwa wakati.Hizi ni hela za ziada kwa hiyo inatakiwa tujipange vizuri ili tuweze kutekeleza yale yaliyo kwenye bajeti pamoja na haya ya ziada.Kazi zote zinatakiwa ziende kwa pamoja ili ifikapo mwezi desemba madarasa yote yawe yamekamilika” Alisema Katibu Tawala.
Wakitoa taarifa ya mpango kazi wa maandalizi ya awali ya namna ya utekelezaji wa ujenzi vyumba hivyo vya madarasa; Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Wang’ing’ombe Maryam Muhaji , Mkurugenzi wa Wilaya ya Makete William Makufwe , Mkurugenzi wa Wilaya ya Ludewa Sunday Deogratias, Mkurugenzi wa Wilaya ya Njombe Sharifa Nabalang’anya, Mkurugenzi wa Mji Makambako Kenneth Haule na Kaimu Mkurugenzi Halmashuri ya Mji Njombe Shigela Ganja wamesema kuwa mpaka sasa wapo tayari kuanza kazi na pia taratibu zote muhimu zimeshaanza kufanyika ikiwa ni pamoja na kupeleka maombi kwa ajili ya mapitio ya bajeti,kufufua kamati za ujenzi pamoja na kupeleka taarifa kwa barua kwenda ngazi za chini wakiwemo Watendaji na Wakuu wa Shule pamoja na maeneo yote yenye miradi kwa ajili ya maandalizi ya ujenzi.
Deo Mwanyika Mbunge wa jimbo la Njombe Mjini na Deo Sanga Mbunge wa Jimbo la Makambako wamemshukuru Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa anayoifanya ya ujenzi wa vyumba vya madarasa jambo ambalo linawapunguzia Wananchi mzigo mzito wa uchangiaji na badala yake kuweka nguvu katika shughuli nyingine.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Njombe Jassel Mwamwala amesema kuwa majengo yatakayojengwa yazingatie ubora na pia amewataka viongozi wa Chama kuhakikisha kuwa ngazi zote za chama wanashirikiana na Watendaji bila migongano na kuhakikisha kuwa kumbukumbu zote muhimu za ujenzi zinatunzwa sahihi.
Antony Mtaka Mkuu wa Mkoa wa Njombe amesema kuwa dhamira yake kubwa ni kuhakikisha kila mtu anashiriki ipasavyo kwenye usimamizi wa miradi hii toka hatua za awali ili kushirikishana na kuweza kwenda kwenye utekelezaji kwa pamoja.
“Itakuwa ni jambo la kushangaza tunashindwa kumaliza madarasa na unapoteza kazi na fedha zipo kwenye akaunti. Wakati mwingine tunapoteza thamani yetu na heshima zetu na baadaye kudharaulika kwa tama ndogondogo ambazo hazina manufaa. Jenga darasa zuri ambalo litakupa sifa. “Alisema Mtaka
Aliendelea kusema “Mkoa wa Njombe tumepatiwa Bilioni 1.96. Dhamira yetu ni kuwa Mkoa wa kwanza kukamilisha madarasa kwa wakati. Na ili kujitofautisha na wengine ndani ya siku 75 tunapokwenda kuanza utekelezaji wa kazi hii siku moja kabla ya maadhimisho ya siku ya UKIMWI duniani tuwe tumekamilisha madarasa yote. ”Alisema Mtaka
Katika hatua nyingine Mtaka amezitaka Timu za Menejimenti za Halmashauri kujipambanua, kuwa na mawazo tofauti zaidi juu ya matumizi ya asilimia 40 za maendeleo kwa kuwa na miradi ya kipekee na kitofauti badala ya kuwa na mawazo yaleyale yanayofanyika katika ngazi Vijiji na Kata.
Kwa upande wa Halmashauri ya Mji Njombe imepokea kiasi cha shilingi milioni 520 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba 26 vya madarasa kazi ambayo ina kwenda kuanza mara moja.
Ofisi yetu inapatikana barabara ya Njombe-Songea mtaa wa Mjimwema.
Sanduku la Posta: S.L.P 577
Simu ya Mezani: 026-2968833
Simu ya Mkononi: 026-2968833
Barua Pepe: td@njombetc.go.tz
Haki Miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Njombe