Mkuu wa Wilaya ya Njombe akiwa ameongozana na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Njombe Erasto Mpete,Katibu Tawala Wilaya George Emmanuel na Mkurugenzi wa Halmashuri ya Mji Njombe Kuruthum Sadick wamekutana na uongozi wa Mji rafiki wa Milternberg Nchini ujerumani na wafadhili wa mradi rafiki wa mazingingira ujulikanao kama “Climate Partnership” na kuwasilisha andiko kuhusu uboreshaji wa mazingira ya Mji wa Njombe kwa kuwezesha ujenzi wa dampo la kisasa na kuifanya Njombe kuwa safi na Kijani.
Akiwasilisha andiko hilo Mjini Milternberg Ujerumani Katibu Tawala Wilaya ya Njombe George Emmanuel alisema kuwa kupitia ziara ambayo alishiriki awali iliyopelekea kuja na andiko hilo jambo la kipekee waliloweza kujifunza ni namna bora ya utenganishaji na uhifadhi taka kutoka kwa wazalishaji taka,ukusanyaji na uchakataji taka na kuzalisha bidhaa kama mbolea na umeme jambo ambalo wao wameliona linafaa kufanyika pia katika Mji wa Njombe na kuachana na utaratibu unaotumika sasa wa kukusanya taka kwa pamoja na kupeleka dampo.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Njombe Kissa Gwakisa akiwasilisha salamu za Serikali ya Tanzania amesema kuwa Serikali imekua ikihamasisha urafiki baina ya Nchi mbalimbali kwa lengo la kubadilishana uzoefu, kujifunza, kutafuta wadau kwenye uwekezaji na pia kutangaza vivutio mbalimbali vya utalii vilivyopo Nchini Tanzania ili kuiletea Nchi Maendeleo.
Kissa alisema kuwa Serikali ya Tanzania kupitia Filamu ya “THE ROYAL TOUR” mhusika mkuu akiwa ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanznaia Samia Suluhu Hassan iliandaliwa lengo ikiwa ni kuonesha vivutio mbalimbali vilivyopo Nchini, kuvitangaza na kuhamasisha Watalii kutoka Nchi mbalimbali duniani kuweza kuja Tanzania kutembelea vivutio hivyo vya kipekee na hivyo kuwataka kutumia fursa hiyo kuvitembelea vivutio hivyo.
Kuhusu usafi wa mazingira Kissa amesema kuwa Tanzania iliweka utaratibu wa kuhakikisha kuwa kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi inatumika kwa shughuli za usafi ili kuendelea kuwajengea Wananchi utamaduni wa kufanya usafi na utunzaji wa mazingira.
Mara baada ya kuwasilisha andiko hilo lililobeba ujumbe muhimu wa kuifanya Njombe kuwa safi na kijani matarajio ni Njombe kunufaika kwa kupata dampo kuu kubwa na la kisasa na pia Wananchi wake kujengewa uwezo wa njia bora za uhifadhi taka kwa kuzitenganisha kuanzia majumbani mpaka kufikia eneo la dampo zitakapokuwa zinachakatwa.
Ofisi yetu inapatikana barabara ya Njombe-Songea mtaa wa Mjimwema.
Sanduku la Posta: S.L.P 577
Simu ya Mezani: 026-2968833
Simu ya Mkononi: 026-2968833
Barua Pepe: td@njombetc.go.tz
Haki Miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Njombe