Akizungumza mara baada ya kutembelea na kukagua shamba la Mkulima wa Parachichi Steven Mlimbila kutoka kikundi cha Tuondoke kinachojishughulisha na kilimo hicho, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali imedhamiria kuboresha kilimo cha Parachichi kwani thamani na uhitaji wa zao hilo nje ya nchi umekuwa ni mkubwa ilihali uzalishaji wake bado ni mdogo.
“Zao la Parachichi ni miongoni mwa mazao yenye faida kubwa na gharama za uzalishaji ni nafuu. Niwahimeze Wananchi kulima kwa ajili ya kujipatia pesa. Ukitaka kuwekeza kwa mtoto wako kwa ajili ya shule lima parachichi. Parachichi ni pesa.”Alisema Waziri Mkuu.
Waziri Mkuu ameziagiza Halmashauri zote za Mkoa wa Njombe zinazolima zao la parachichi kupitia fedha za asilimia 10 zianzishe vitalu vya kuotesha miche katika eneo la kuanzia ekari tatu na kuigawa bure kwa wakulima, lengo likiwa ni kuhamasisha wananchi wengi kulima zao hilo na kuongeza uzalishaji
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Serikali inatarajia kujenga chumba maalumu cha kuhifadhi baridi katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Songwe kwa ajili ya kuhifadhia maparachichi pamoja na mazao mengine kabla ya kusafirishwa kwenda nje ya nchi.
Awali akitoa taarifa ya uzalishaji wa zao la Parachichi katika Mkoa wa Njombe Mkuu wa Mkoa wa Njombe Mhandisi Marwa Rubirya amesema kuwa kwa kipindi cha mwaka jana wakulima 9130 waliweza kulima parachichi na kuzalisha tani 7100 pekee kwa kipindi cha mwaka mmoja.
Kufuatia umuhimu wa zao hilo, Waziri Mkuu amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Mhandisi Marwa Mwita Rubirya afuatilie maendeleo ya vikundi vya wakulima wa parachichi na kushirikiana nao katika kutatua changamoto zinazowakabili.
Waziri Mkuu amempongeza Bw. Mlimbira kwa kuwa na shamba kubwa la parachichi ambalo limewezesha kutoa ajira kwa wananchi wengi pamoja na kuwahamasisha walime zao kwa kuwagawia miche kwa gharama nafuu.
Kwa upande wake, Bw. Mlimbira amesema ekari moja hupandwa miti 64 ya parachichi kwa nafasi ya mita nane kwa mita nane na mche mmoja huuzwa kati ya shilingi 2,000 hadi 5,000 kwa kutegemea na ukubwa wa mche.
Amesema mti mmoja wa parachichi unatoa kiasi cha wastani wa kilo 150 hadi 500 ambapo inakadiriwa kuzalisha parachichi zenye thamani ya shilingi 200,000 hadi 750,000 kwa mti wenye umri wa miaka mitano hadi 10 na huanza kuzaa baada ya mwaka mmoja na nusu hadi miaka mitatu.
Ofisi yetu inapatikana barabara ya Njombe-Songea mtaa wa Mjimwema.
Sanduku la Posta: S.L.P 577
Simu ya Mezani: 026-2968833
Simu ya Mkononi: 026-2968833
Barua Pepe: td@njombetc.go.tz
Haki Miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Njombe