Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Njombe Kuruthum Sadick leo amepokea Ugeni uliohusisha Wawakilishi kutoka katika Vyuo Vikuu vinne Nchini CANADA, lengo ikiwa ni kutambulisha programu iitwayo “Ndoto yangu ni dhahabu” itakayowawezesha Wanawake na Vijana wa Kike kupata elimu kupitia mafunzo ya kiufundi, kukuza vipaji vyao, kujengewa uwezo juu ya usawa wa kijinsia na kukabiliana na ukosefu wa ajira.
Jacqueline Towell Meneja wa Miradi na Mahusinao ya Kimataifa kutoka Kampasi la Oshawa Nchini Canada amesema kuwa Mpango huo wa uwezeshaji ufundi stadi unaotekelezwa na Umoja wa Vyuo Vikuu vya Canada Kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu ya Sayansi na Teknolojia ya Tanzania kupitia Idara ya Elimu na Ufundi Stadi (VETA), Chuo Cha Maendeleo Njombe, Shirika la COCODA na Maafisa Maendeleo wa Halmashauri utatekelezwa kwa kipindi cha miaka 7 kuanzia mwaka 2021-2028, ambapo katika miaka 4 ya kuanza kwa programu hiyo timu ya Wataalamu kutoka Nchini Canada watashirikiana kufanya kazi kwa pamoja na kubadilishana uzoefu katika maeneo mbalimbali ikiwemo usawa wa kijinsia, haki za binadamu, mazingira, afya na usalama na masoko.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Njombe Kuruthum Sadick amepongeza hatua hiyo kubwa ya Kimaendeleo na amesema kuwa programu hiyo ni muhimu hususani kwa Vijana wa Kike ambao walishindwa kuendelea na Shule kutokana na kupata Ujauzito na wengine sababu mbalimbali za kimaisha na kupelekea kushindwa kuendelea na mfumo rasmi wa elimu ambao kwa sasa wapo katika Vyuo hivyo vya Maendeleo. Kuruthum amesema kuwa programu hiyo itawasaidia katika kuongeza ubunifu na ufanisi zaidi katika shughuli watakazokuwa wanazifanya kupitia programu hiyo.
Ofisi yetu inapatikana barabara ya Njombe-Songea mtaa wa Mjimwema.
Sanduku la Posta: S.L.P 577
Simu ya Mezani: 026-2968833
Simu ya Mkononi: 026-2968833
Barua Pepe: td@njombetc.go.tz
Haki Miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Njombe