Wakizungumza kwa wakati tofauti Mawaziri walioambata na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Ziara yake Mkoani Njombe wamesema kuwa yapo mambo mengi ambayo yamefanyika kwa muda mfupi ambao Wananchi wa Tanzania inabidi kujivunia.
Dkt. Pindi Chana Waziri wa Maliasili na Utalii amesema kuwa kupitia program ya "The Royal Tour" Tanzania imefunguka na imekua ikipokea wageni kutoka mataifa mbalimbali kote duniani. "Wageni hawa wanapokuja Tanzania siyo tu kwakuwa Tanzania ipo kwenye ramani, lakini pia suala la uongozi bora, siasa safi na uhuru wa kisiasa chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan.Zipo nchi zingetamani sana kupata wageni kama Tanzania lakini wakiangalia nchi hizo hazijatulia kwa mapigano, hazijatulia kisiasa – hata ukisema wageni waje inakuwa si rahisi"Amesema Pindi Chana
Akizungumza kuhusu hali ya utalii kwa upande wa nyanda za juu kusini Waziri amesema kuwa kwa sasa idadi ya Watalii imeongezeka ambapo takwimu zinaonesha Ruaha National Park watalii wametoka takribani 9000 mpaka 1300 na Kitulo watalii sasa hivi hawapungui 1200.
Waziri wa Kilimo Hussein Bashe amesema kuwa mnamo tarehe 08 Rais Samia alizindua skimu ya kutoa ruzuku ya mbolea ambapo Mkoa wa Njombe unamawakala wengi wa mbolea. Waziri Bashe amewataka Mawaka la hao kuwa bei ya mbolea iliyozinduliwa na Mh. Rais na ambayo itatangazwa kwa kupitia magazeti na televisheni, itakayoanza tarehe 15 mwezi wa 8. Bei hiyo ni moja kuanzia Dar es Salaam mpaka mwisho wa Tanzania ikiwa kijijini au mjini.
Hamad Masauni Waziri wa mambo ya ndani amesema kuwa Serikali inakuja na Mpango kabambe wa kuboresha makazi ya Polisi na Ofisi ambapo kwa Njombe licha ya kuwa kituo Cha kisasa umefanyika katika Wilaya ya Wang'ing'ombe, Serikali pia inaendelea na Ujenzi wa ghorofa kwa ajili ya makao makuu ya polisi.
Waziri wa Afya Ummy Mwalimu amesema kuwa Wizara yake imekusudia kupunguza gharama za kupata matibabu nchini ili kuwapunguzia mzigo Watanzania kwa kulipa fedha nyingi kwa ajili ya kupata huduma katika hospitali zetu ikiwa ni pamoja na gharama za kumuona daktari ikiwa gharama za sasa ni Shilingi 15000 jambo ambalo linafanyiwa tathmini.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan akizungumza katika mkutano huo ameipongeza Halmashauri kwa kuendelea kukusanya mapato ya Halmashauri vizuri na ametaka jitihada zaidi kuongezwa kwenye ukusanyaji wa mapato ya Halmashauri kwani uwezo wa kukusanya zaidi upo. Rais Samia amewataka Viongozi kufanya Kazi kwa bidii na kuwatumika Wananchi na pia Wananchi kuhakikisha wanatoa ushirikiano wa kutosha kwa viongozi wao ili kufikia malengo kusudiwa.
Ofisi yetu inapatikana barabara ya Njombe-Songea mtaa wa Mjimwema.
Sanduku la Posta: S.L.P 577
Simu ya Mezani: 026-2968833
Simu ya Mkononi: 026-2968833
Barua Pepe: td@njombetc.go.tz
Haki Miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Njombe