Na,Ichikael Malisa
Katika kuhakikisha kuwa sekta ya mifugo inakuwa endelevu na yenye tija kwa wafugaji, Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imeanza rasmi kutoa ruzuku ya chanjo kwa mifugo ili kudhibiti magonjwa yanayoweza kuzuilika na hivyo kupunguza hasara kwa wafugaji.
Chanjo ni njia salama, rahisi na yenye ufanisi mkubwa wa kuzuia magonjwa kwa wanyama. Magonjwa haya mfano homa ya mapafu kwa ng’ombe,kideri,mafua makali kwa kuku na ndui kama yasipozuiwa mapema, huweza kuathiri uzalishaji, kuleta vifo kwa wanyama na hatimaye kuwasababishia wafugaji hasara kubwa kiuchumi.
Halmashauri ya Mji Njombe imepokea ruzuku ya chanjo dozi 227,000 kwa ajili ya kuwahudumia wafugaji wa maeneo mbalimbali ndani ya halmashauri,zoezi ambalo tayari limeanza kutekelezwa na Julai 4, 2025, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dkt.Edwin Mhede alifanya uzinduzi wa kutoa chanjo na kuweka alama ya utambuzi kwa mfugaji mmoja wa mfano, Bwana Joseph Kimwayeya,ambapo jumla ya ng’ombe 11 na kuku 11 walichanjwa.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Dkt.Mhede, alieleza kuwa hatua ya Serikali kutoa ruzuku kwenye chanjo za mifugo ni mwendelezo wa mkakati wa Serikali kusaidia sekta ya mifugo kama ambavyo imekuwa ikifanyika kwa sekta ya kilimo. "Mmeona Serikali mara kadhaa imeleta pembejeo ya mbolea na mbegu, sasa hatuishii huko zote hizi ni sekta za uzalishaji ndiyo maana sasa tumekuja kwenye mifugo." alisema Dkt. Mhede.
Kwa mujibu wa mpango huu unaoendelea nchi nzima ,chanjo ya kuku aina ya tatu moja ambayo itamkinga kuku dhidi ya ugonjwa wa kideri Newcastle),ndui (fawl pox) na mafua makali ( infectious coryza zinatolewa bure kabisa kwa wafugaji nchi nzima , huku kwa upande wa ng’ombe mfugaji akichangia kiasi kidogo cha shilingi 500 tu kwa chanjo dhidi ya homa ya mapafu kwa kila dozi, gharama ambayo ni ndogo ukilinganisha na hasara inayoweza kutokea endapo mifugo haitachanjwa.
Wafugaji katika Halmashauri ya Mji Njombe wamepokea mpango huu kwa furaha na shukrani, wakieleza kuwa hatua hiyo ya Serikali ni ya kupongezwa na itawasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza vifo vya mifugo, kuongeza uzalishaji na kuboresha kipato cha kaya.
"Nashukuru Serikali kwamba imetoa punguzo la chanjo hii ,imetupungizia sana gharama sisi wakulima wa kipato cha chini,tunashukuru kwa pembejeo tunazozipata kwenye kilimo na mifugo tunaomba serikali iendelee kutusaidia wakulima"Alisema Joseph Kimwayeya-Mfugaji Mtaa wa Lunyanywi.
Tarehe 16 Juni 2025, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, alizindua rasmi chanjo za magonjwa matano ya kipaumbele ikiwa ni pamoja na homa ya mapafu, sokota ya mbuzi (PPR), ndui ya kuku (fowl pox), mafua makali ya kuku (infectious coryza), na kideri (Newcastle disease).
Wafugaji wote wanahimizwa kuhakikisha mifugo yao inapatiwa chanjo kwa wakati ili kulinda afya ya mifugo na kuepuka maambukizi ya magonjwa. Aidha, mnakumbushwa kuwa chanjo ni uwekezaji bora katika ustawi wa mifugo kwa uchumi wa mfugaji mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.
Ofisi yetu inapatikana barabara ya Njombe-Songea mtaa wa Mjimwema.
Sanduku la Posta: S.L.P 577
Simu ya Mezani: 026-2968833
Simu ya Mkononi: 026-2968833
Barua Pepe: td@njombetc.go.tz
Haki Miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Njombe