Halmashauri ya Mji Njombe imepokea jumla ya pikipiki 13 zenye thamani ya shilingi milioni 39 kwa waratibu elimu Kata 13 lengo ikiwa ni kufanya ufatiliaji na usimamizi wa elimu katika Kata.
Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo Mwakilishi kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI Salum Mkuya amesema kuwa serikali ya awamu ya tano imedhamiria kuboresha sekta ya elimu kwa kuhakikisha kuwa wasimamizi wa elimu wanawezeshwa upatikanaji wa vitendea kazi ili kufanya mazingira ya kazi kuwa rafiki.
“Pikipiki hizi zikafanye kazi ya ufuatiliaji kwa kupandisha kiwango cha ufaulu, kuhakikisha wanafunzi wanajua kusoma na kuandika ikiwa ni sambamba na kuthibiti utoro mashuleni.”Alisema Mkuya
Aidha, Mkuya ameiomba Halmashauri kuhakikisha kuwa pikipiki zote zilizokabidhiwa zinapatiwa bima kama serikali ilivyoagiza.
Naye mwenyekiti wa Halmashauri Edwin Mwanzinga amesema kuwa anaishukuru serikali ya CCM kupitia kwa Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Magufuli kwa kutambua umuhimu wa pikipiki hizo kwa waratibu elimu kwani itarahisisha shughuli za usimamizi na ufuatiliaji elimu hususani katika Halmashauri ambazo maeneo mengi jiografia yake ni ngumu kufikika kutokana na ukubwa wa eneo halikadhalika changamoto za miundombinu.
“Najua waratibu mlikua mnafanya kazi katika mazingira magumu niwaombe sasa tukafanye kazi bila visingizio na ni lazima tuwe wa kwanza kimkoa kwa sababu tumepata vitendea kazi. Lakini niwaombe sana mkazitunze pikipiki hizi ili tuweze kwenda nazo kwa muda mrefu. Kwa wale ambao hamjui kuzitumia tusitumie pikipiki hizi kujifunzia. Ni imani yangu mtaenda kujifunza mpate leseni na muweze kuzitumia vizuri na kwa tahadhari” Mwanzinga alisema
Akitoa salamu za shukrani kwa niaba ya waratibu elimu Ester Mjuu Mratibu Elimu Kata ya Ramadhani Halmashauri ya Njombe alisema kuwa sasa wataweza kufika kila kona ya Kata zao katika kufuatilia usimamizi wa elimu.
“Tunashukuru sana kwa vitendea kazi hivi,miongoni mwa changamoto iliyokuwa inatukabili imepata ufumbuzi tutaenda kufanya kazi kwa kadri mlivyotuelekeza ili kuhakikisha kuwa tunakuwa na Taifa la wasomi kwa kufanya ufuatiliaji na usimamizi wa karibu kwenye sekta ya elimu.”Alisema
Ofisi yetu inapatikana barabara ya Njombe-Songea mtaa wa Mjimwema.
Sanduku la Posta: S.L.P 577
Simu ya Mezani: 026-2968833
Simu ya Mkononi: 026-2968833
Barua Pepe: td@njombetc.go.tz
Haki Miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Njombe