Kituo cha Rasilimali za Kilimo kilichopo kijiji cha Kisilo, kata ya Lugenge, Halmashauri ya Mji wa Njombe, ni miongoni mwa vituo vitakavyonufaika na matrekta mapya yaliyoletwa na Serikali kwa lengo la kusaidia wakulima kuhamia kwenye kilimo cha kisasa chenye tija.
Kauli hiyo imetolewa tarehe 21 Desemba 2024 na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo, Mheshimiwa Deo Philip Mwanyika, alipoongoza kamati hiyo kutembelea na kukagua rasilimali zilizopo kituo hicho.
Mheshimiwa Mwanyika amesema Serikali inatambua mchango wa sekta ya kilimo kwa pato la taifa, na kwamba mbali na ruzuku ya mbolea na viuatilifu, sasa inatoa zana za kisasa, zikiwemo matrekta, ili wakulima wapate fursa yakukodisha kwa gharama nafuu.
"Nimefurahi kusikia namna kituo hiki kimewanufaisha watu wengi. Ni lazima tufanye maboresho. Wakulima sasa hamna haja ya kununua matrekta kwa gharama kubwa, kwani Serikali inatoa matrekta, na hapa Njombe tayari yamefika yatakuja hapa kisilo". alisema Mheshimiwa Mwanyika.
Kamati hiyo, kupitia mwenyekiti wake, ilitoa maelekezo ya kufanya maandalizi ya mapokezi ya matrekta hayo kwa kuhakikisha eneo hilo linawekewa uzio kwa ajili ya ulinzi wa zana hizo.
Kwa upande wao, wananchi wa kijiji cha Kisilo, akiwemo Kalo Mligo na Frank Mwabena, wameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kupitia kamati hiyo, kwa kutambua umuhimu wa vituo kama hivyo ambavyo vimekuwa msaada mkubwa kwa wakulima na wafugaji.
"Kituo hiki kimekuwa msaada mkubwa. Kupitia kituo hiki nilihamasika kufuga ng'ombe. Kinawasaidia wananchi wengi, siyo tu wa kijiji cha Kisilo, bali wa Halmashauri nzima kwa ujumla," alisema Frank Mwabena, mkazi wa Kisilo.
Kituo cha Zana za Kilimo cha Kisilo kilianzishwa mwaka 2003 chini ya Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine kwa lengo la kuibua na kueneza teknolojia mpya za kilimo kwa nadharia na vitendo. Kituo hiki kimewqsaidia wananchi kuzalisha mazao kama mahindi, ngano, viazi, na maharagwe, kwa kutumia zana bora za kilimo, huku kikifanya tafiti na majaribio ya zana na mbegu bora ili kusaidia wakulima kutumia mbegu bora na kuondokana na matumizi ya jembe la mkono.
Ofisi yetu inapatikana barabara ya Njombe-Songea mtaa wa Mjimwema.
Sanduku la Posta: S.L.P 577
Simu ya Mezani: 026-2968833
Simu ya Mkononi: 026-2968833
Barua Pepe: td@njombetc.go.tz
Haki Miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Njombe