Mkoa wa Njombe umepokea jumla ya vitabu elfu 30355 kwa ajili ya masomo ya Hisabati, Kiingereza, Kiswahili, Maarifa na Uraia huku Halmashauri ya Mji Njombe ikipatiwa jumla ya vitabu elfu 4634 ikiwa ni vitabu vya kiada kwa ajili ya wanafunzi wa darasa la nne.
Akizungumza wakati wa makabidhiano ya vitabu hivyo yaliyofanyika katika Ofisi za Halmashauri ya Mji Njombe, mwakilishi wa Ofisi ya Rais TAMISEMI Salum Mkuya alisema kuwa vitabu hivyo vinavyosambazwa Nchi nzima katika Halmashauri zote vinalenga kuimarisha sekta ya elimu kwa upande wa Shule za Msingi, kama ilivyoainishwa katika Ilani ya CCM ya mwaka 2015-2020.
“Mtaona nyie wenyewe kwenye elimu bila malipo, fedha za uendeshaji, posho za wakuu wa shule na waratibu elimu kata, ujenzi wa madarasa na madawati haya yote yanafanywa na Mhe. Rais John Pombe Magufuli hatuna budi kumuombea kwa mabadiliko haya anayofanya kwa kuandika historia ya Tanzania mpya na inaonesha ni kwa jinsi gani utekelezaji wa Ilani unafanyika kwa kasi kubwa.”Alisema Mkuya
Aidha, Mkuya amewaomba viongozi wa Mkoa, wasimamizi wa elimu katika ngazi za Halmashauri na waalimu kuhakikisha kuwa vitabu hivyo vinatunzwa na vinatumika ipasavyo kwani ni haki ya watoto kupata elimu bora na serikali itaendelea kuboresha sekta ya elimu mpaka maendeleo yapatikane.
Akipokea vitabu hivyo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Mkuu wa Wilaya ya Njombe Bi. Ruth Msafiri alisema kuwa amefurahishwa sana na upatikanaji wa vitabu hivyo na inaonesha waziwazi ni kwa jinsi gani Mhe. Rais anatekeleza ahadi zake kwa wakati pindi anapotamka jambo.
Kwa wakati huo huo Mkuu huyo wa Wilaya Amempongeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Njombe Illuminatha Mwenda kwa kusimamia vyema sekta ya elimu kwani Halmashauri ya Mji Njombe imekua ikiongoza Kimkoa katika mitihani ya Kitaifa kwa upande wa Shule za Msingi na Sekondari huku ufaulu wa Kimkoa ukiwa ni wa daraja A.
Antony Katani ni Katibu CCM Wilaya ambaye yeye amempongeza Rais kwa kutafsiri kwa vitendo utekelezaji wa ilani hususani kwenye sekta ya elimu kwa kuhakikisha uimarishaji wa sekta hiyo ikiwa ni sambamba na upatikanaji wa vitabu vya kutosha mashuleni.
Katani pia amewataka wale wote wanaobeza mpango wa serikali kutoa elimu bila malipo kupuuzwa kwani hawana nia njema na serikali ya awamu ya tano.
“Kwa Mtanzania yeyote mwenye nia njema na Nchi hii hapa ndipo tulipokuwa tunapahitaji,na tunaamini kuwa Mhe. Rais atatupeleka mahali ambapo wengi tulikuwa tunapahitaji. Wale wote wanaobeza jitihada za makusudi anazofanya Mhe. Rais kwa upande wa elimu bila malipo tuwapuuze na Mwenyezi Mungu awalaani” Alisema Katani
Nae mwakilishi wa wanafunzi kutoka shule ya Msingi Ruhuji B John Mwanyika ameishukuru serikali kwa kupatiwa vitabu hivyo na amesema kupitia vitabu hivyo walivyopokea leo vitawawezesha wao kusoma kwa bidii na wanaahidi kufanya vizuri katika masomo yao kwani tatizo la uhaba wa vitabu katika masomo yote sasa umepata ufumbuzi na kufikia kikomo.
Ofisi yetu inapatikana barabara ya Njombe-Songea mtaa wa Mjimwema.
Sanduku la Posta: S.L.P 577
Simu ya Mezani: 026-2968833
Simu ya Mkononi: 026-2968833
Barua Pepe: td@njombetc.go.tz
Haki Miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Njombe