Wananchi katika Halmashauri ya mji wa Njombe wametakiwa kuongeza juhudi za kuchangia michango ya utoaji taka ngumu katika maeneo yao kwani bila kufanya hivyo mji utakuwa na taka ambazo zinaweza kuwasababisha magonjwa ya mlipuko na kuwaingiza kwenye gharama kubwa ya matibabu.
Kauli hiyo imetolewa na Afisa mazingira wa halmashauri ya mji wa Njombe Nelson Mlwisa wakati uongozi wa Halmashauri hiyo chini ya mkurugenzi mtendaji ulipofika na kushiriki zoezi la usafi katika soko kuu jipya mjini Njombe ikiwa ni miongoni mwa shughuli zinazofanyika kuelekea siku ya uhuru wa Tanganyika hapo Disemba 9 mwaka huu.
Adily Mwakyusa ni makamu mwenyekiti wa soko kuu ambaye anasema wamekuwa na utaratibu wa kufanya usafi ndani ya soko hilo hivyo hawategemee kutokea kwa magonjwa yoyote ya mlipuko kwa kuwa usafi ni jadi ya Wananchi wa mkoa mzima wa Njombe.
Joyce Kilumile na Magreth Msigwa ni wakazi wa Njombe ambao wamekiri kufurahishwa na hatua ya uongozi wa Halmashauri ya mji wa Njombe kushiriki nao kufanya usafi na kwamba hiyo inasaidia sana kuwaepusha na magonjwa ya kipindupindu hasa wakati wa mvua.
Kwa upande wake mkurugenzi wa Halmashauri ya mji wa Njombe Kuruthum Sadick amesema ni muhimu wananchi wakaendelea kudumisha uhuru tulioupata kwa mkoloni ili taifa liendelee kuwa na amani.Disemba 9 mwaka huu Tanzania inatimiza Miaka 61 tangu ipate uhuru wake toka kwa muingereza ambapo mikoa mbalimbali inaadhimisho kumbukizi hii kwa kufanya shughuli mbalimbali za kijamii.
Ofisi yetu inapatikana barabara ya Njombe-Songea mtaa wa Mjimwema.
Sanduku la Posta: S.L.P 577
Simu ya Mezani: 026-2968833
Simu ya Mkononi: 026-2968833
Barua Pepe: td@njombetc.go.tz
Haki Miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Njombe