Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) taifa Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi, ametoa wito kwa watendaji wa ngazi mbalimbali za Serikali, kuwajibika na kusimamia vizuri fedha zinazotolewa na serikali kwa ajili ya miradi ya mdeleo ili thamani ya fedha hizo ionekane.
Dkt. Nchimbi amesema hayo tarehe 18 Aprili, 2024 wakati akizungumza na wananchi mjini Makambako kwenye mkutano wa hadhara.
"Nimesikia hapa, Mkoa wa Njombe umepewa shilingi bilioni 900, nimesisimka kwasababu hizi ni hela nyingi sana,” alisema na kuongeza kuwa, “niwasisitize wafanyakazi wote wa Serikali kuwa waaminifu katika usimamizi wa fedha za miradi zinazotolewa na Serikali zitumike vizuri."
Aidha, amevitaka vyombo vya usalama ikiwemo Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kuisaidia Serikali kwa kuzuia wabadhilifu wa mali za umma na kufanya kazi ya kuzuia badala yakusubiri kukamata wahalifu.
"TAKUKURU tusisubiri kukamata walioiba, tuzie wezi wa mali ya umma wabadhirifu na wala rushwa kwa kufuatilia fedha zinazotolewa katika miradi mikubwa tangu inapoanza.''
Katika hatua nyingine, Katibu Mkuu huyo wa CCM, amewakumbusha wananchi wote kuwajibika kwa taifa lao kwa kuwa waadilifu na wazalendo.
"Kila mmoja wenu ajitahidi kuwa mwema kwenye jamii, usiwe tapeli, usitoe rushwa, usiwe mwizi, lipende taifa lako, haya mambo yasiyofaa hayajengi nchi yetu, wote tuungane tuijenge Tanzania yetu, nchi yetu bado changa lakini inaweza kujengwa na Watanzania wakiamua kufanya mambo kwa kuipenda nchi yetu."
Ziara ya Katibu wa CCM mkoani Njombe imenza Aprili 18, 2024 na itahitimishwa Aprili 19, 2024 Mjini Njombe ambapo atafanya mkutano wa ndani na watendaji mbalimbali wa Chama na kupokea taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi kwa Mkoa wa Njombe.
Ofisi yetu inapatikana barabara ya Njombe-Songea mtaa wa Mjimwema.
Sanduku la Posta: S.L.P 577
Simu ya Mezani: 026-2968833
Simu ya Mkononi: 026-2968833
Barua Pepe: td@njombetc.go.tz
Haki Miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Njombe