Na Ichikael Malisa.
Serikali imeagiza Mikoa yote ya Nyanda za juu kusini kuhakikisha inaainisha na kutangaza maeneo ya utalii sambamba na fursa za uwekezaji zinazopatikana ndani ya mikoa hiyo ili kuendeleza na kukuza sekta ya utalii nchini.
Kauli hiyo imetolewa Septemba 28,2023 na Naibu waziri wa Viwanda na Biashara Mhe Exaud Kigahe katika viwanja wa Kihesa kilolo Mkoani Iringa wakati akifunga Maonesho ya Utalii Karibu Kusini mwaka 2023.
"Kila mkoa uhakikishe unaibua maeneo mapya ya utalii na kutangaza vivutio vyake na fursa za Uwekezaji ndani ya mkoa maana tunaelewa utalii unaenda sambamba na uwekezaji hivyo ni vyema kujiandaa kupokea wawekezaji pia"alisema Naibu Waziri Kigahe.
Mhe Kigahe alisema kuwa serikali na taasisi zake itaendelea kufanya kazi yakutangaza vivutio vya utalii pamoja na kuhakisha mazingira rafiki kwenye sekta ya utalii yanaendelea kuboreshwa ili kuwavutia watalii wengi zaidi.
"Serikali inaendelea kuboresha miundombinu pamoja na kuendelea kutangaza vivutio vya utalii vinavyopatikana ukanda huu kwa kuwa utangazaji ni nguzo muhimu ya kukuza utalii kusini mwa Tanzania"alisema.
Aidha alitumia fursa hiyo kuwakaribisha wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kufika na kuwekeza kwenye mikoa ya nyanda za juu kusini,pamoja na kuhakikisha mikoa yote inajipanga kwa kuweka mazingira rafiki kabla mwekezaji hajafika.
"Endeleeni kuandaa na kuanisha maeneo yote yanayofaa kwa uwekezaji,kamilisheni taratibu zote za msingi zinazotakiwa kama ni kulipa fidia ili mwekezaji anapofika akute maandalizi yapo tayari"alisema Naibu Waziri Kigahe.
Hata hivyo alisema maonesho ya utalii karibu kusini yana tija kubwa kwa uchumi wa mikoa ya kusini mwa Tanzania hasa kwenye kufanya biashara yakuwahudumia wageni wanaofika kwa ajili ya maonesho hayo.
"Tuendelee kuwekeza kwenye nyumba za kulala wageni na biashara nyingine, ili tuwe kwenye nafasi yakuweza kupokea na kuvutia wawekezaji wengi zaidi"alisema.
Maonesho ya utalii karibu kusini yalidumu kwa takribani siku sita kuanzia Septemba 23,2023 na yalibeba kauli mbiu inayosema "Utalii karibu kusini mwelekeo mpya wa uwekezaji"
Ofisi yetu inapatikana barabara ya Njombe-Songea mtaa wa Mjimwema.
Sanduku la Posta: S.L.P 577
Simu ya Mezani: 026-2968833
Simu ya Mkononi: 026-2968833
Barua Pepe: td@njombetc.go.tz
Haki Miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Njombe