Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto, imewashukuru waganga wa tiba asili na tiba mbadala kwa ushirikiano katika kuimarisha afya za binaadamu na maendeleo ya jamii kwa ujumla.
Akizungumza na Waganga wa tiba asili na tiba mbadala katika ukumbi wa Halmashauri ya Mji Njombe kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara hiyo,Mwenyekiti wa Timu ya Wataalamu kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto (Idara kuu ya Maendeleo ya Jamii) Bi. Hanifa Selengu amesemu kuwa lengo kuu la wao kufika Mkoani Njombe ni kuunganisha nguvu na Serikali ya Mkoa ili kuweza kupata namna bora ya kukomesha mauaji ya watoto yaliyotokea Mkoani Njombe.
“Lengo la safari yetu ni kuja kuungana na kushiriki na Wataalamu wa Mkoa wa Njombe kwa ajili ya kuona namna ya kuzuia au kuondokana na matatizo haya yanayojitokeza ya ukatili na mauaji kwa watoto.Wizara imetoa tamko kwa waganga wote wa jadi kushirikiana katika kuwafichua waganga wenye kutoa masharti mabaya kwa wanaowahudumia kama wakatafute damu na viungo vya binadamu.”alisema Hanifa
Aidha Wizara imeiomba jamii kuzitumia mamlaka za serikali za Mitaa na jeshi la polisi ili kufichua vitendo vyote viovu vinavyoleta mifarakano miongoni mwao ili hatua stahiki zichukuliwe kwa wakati.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Njombe Bi. Ruth Msafiri amewataka Waganga wa tiba Mbadala na tiba asili katika Halmashauri ya Mji Njombe na wengine Mkoani humo kufanya kazi kwa kufuata utaratibu waliopewa na kuagiza kuondolewa kwa mabango yote mabango yanayotangaza tiba pasipokuwa na kibali maalumu.
“Kama wewe unataka kujitangaza tunakuruhusu lakini fuata taratibu zote za kuhakikisha kuwa tangazo lako linaifikia jamii ulioilenga.Hii ni kwa sababu vibao vingine vyenye matangazo ni vya uchonganishi na mimi sipo tayari kulirihu hili katika wilaya zangu”Alisema Mkuu huyo wa Wilaya.
Akizungumza kwa niaba ya Waganga wa tiba asili Katika Halmashauri ya Mji Njombe Dkt. Mpapai ameishukuru serikali kwa kuwatambua na kuendelea kushirikiana na wataalamu hao,na kuomba elimu zaidi iendelee kutolewa kwao ili kuweza kukumbushana majukumu yao na nidhamu katika kazi.
“Tunahitaji elimu ya kutosha mara kwa mara.Tunapata shida kwa kutokuwa na elimu ya kutosha juu ya majukumu yetu na unakuta tunaweka maslahi mbele.Hakika haya matukio yametuumiza kweli kweli mpaka tumeanza kuishi kwa hofu na familia zetu.”Alisema Dkt. Mpapai.
Kwa upande wake Mwanasheria kutoka Wizara ya afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto (Idara kuu ya maendeleo ya Jamii Bw. Denis Bashaka amesisitiza jamii kufichua vyanzo vinavyosababisha kutokea kwa mauaji hayo na kuangalia namna bora ya kuzifikia jamii kwa kutoa elimu na kuzingatia Sheria, Sera na Miongozo ili kutokomeza vitendo hivyo.
Sambamba na hilo timu hiyo ya Wataalamu kutoka Wizarani ilikutana na kutoa mafunzo kwa kamati zinazojihusisha na ulinzi na usalama wa mtoto katika Halmashauri ya Mji Njombe,Halmashauri ya Wilaya ya Njombe na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na kuwakumbusha wajibu wao katika kuhakikisha usalama wa mtoto na ilifanikiwa kuandaa jumbe maalumu kwa jamii zitakazorushwa kupitia radio za kijamii zikilenga kutoa elimu na kusimamia ulinzi na usalama wa mtoto.
Ofisi yetu inapatikana barabara ya Njombe-Songea mtaa wa Mjimwema.
Sanduku la Posta: S.L.P 577
Simu ya Mezani: 026-2968833
Simu ya Mkononi: 026-2968833
Barua Pepe: td@njombetc.go.tz
Haki Miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Njombe