Viongozi mbalimbali wamesisitiza umuhimu wa vikundi vilivyopatiwa mikopo kutumia fedha hizo kwa malengo yaliyokusudiwa. Haya yamejitokeza katika hafla ya utoaji wa mikopo kwa vikundi katika Halmashauri ya Mji wa Njombe, ambapo jumla ya shilingi bilioni 1.8 zimetolewa kwa vikundi 111 vya wanawake, vijana, na watu wenye ulemavu.
Katibu Tawala wa Wilaya ya Njombe, Bi. Agatha Mhaiki, alieleza kuwa vikundi hivyo vilikidhi vigezo vyote vya kupatiwa mikopo, hivyo ni jukumu lao kuhakikisha fedha zinatumika kwa miradi iliyokusudiwa.
"Tumekopa, tulileta maandiko yenye tija. Naomba fedha tulizopata tuzitumie kama tulivyokusudia," alisisitiza Bi. Agatha.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Njombe, Bw. Samson Medda, aliwasihi wanufaika kuwa waadilifu na kuhakikisha mikopo wanayopata haitumiki kwa matumizi yasiyo na tija. Pia aliwakumbusha kurejesha mikopo kwa wakati ili kutoa fursa kwa wengine kunufaika.
"Mkaitendee haki mikopo hii, fanyeni kazi kwa bidii, zingatieni malengo ya vikundi vyenu. Mikopo hii siyo sadaka, inapaswa kurejeshwa ili wengine nao waweze kufaidika," alisema Bw. Medda.
Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri, Mhe. Nestory Mahenge, alibainisha kuwa vijana mara nyingi wamekuwa kundi linaloshindwa kurejesha mikopo kwa wakati, akiwataka kubadilika ili kufungua fursa zaidi kwa wenzao.
"Mikopo hii tuitumie kama tulivyopanga. Vijana, fedha hizi ni fursa kwa wenye malengo na nidhamu, natamani kuona tukipiga hatua kuelekea kwenye viwanda kupitia mikopo hii," alisema Mhe. Mahenge.
Naye Diwani wa Viti Maalum, Mhe. Angela Mwangeni, aliwataka wanawake waliopokea mikopo kuendelea kuwa mfano mzuri kwa kurejesha kwa wakati.
"Fedha imetolewa kwa wingi kwa wanawake, msiniangushe. Mmeonyesha uaminifu kwa kurejesha vizuri, tuendelee kushirikiana mpaka tumalize marejesho. Vijana, naomba msisite kurejesha mikopo," alisisitiza.
Wanufaika wa mikopo hiyo pia walipata fursa ya kupata elimu ya rushwa kutoka TAKUKURU pamoja na ufafanuzi wa sheria na kanuni za mikopo na adhabu zinazoweza kutolewa endapo vikundi vitashindwa kufanya marejesho.
Ofisi yetu inapatikana barabara ya Njombe-Songea mtaa wa Mjimwema.
Sanduku la Posta: S.L.P 577
Simu ya Mezani: 026-2968833
Simu ya Mkononi: 026-2968833
Barua Pepe: td@njombetc.go.tz
Haki Miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Njombe