Halmashauri ya Mji Njombe kwa kushirikiana na Kampuni ya Lixil ambayo ni watengenezaji wa vyoo aina ya “SATO” imetoa mafunzo kwa mafundi sitini katika kila Kijiji na Mtaa,katika Halmashauri hiyo ili kutimiza lengo la kuhakikisha kuwa kila Taasisi na Kaya inakuwa na vyoo bora na salama.
Akizungumzia lengo la mradi wa uboreshaji vyoo Meneja wa Kampuni ya Lixil Justine Mbowe amesema kuwa wazo hilo lililotokana na jitihada za kuboresha mazingira katika ngazi ya Kaya na Taasisi ambapo kwa mwaka 2018 Kampuni hiyo ilitoa idadi ya vyoo elfu themanini kwa Serikali kupitia wizara ya Afya kupitia kampeni mbalimbali za usafi ikiwemo kampeni ya nyumba ni choo ili Wananchi wenye uhitaji na wa hali ya chini waweze kupata fursa ya kuboresha vyoo vyao na kuwa na mazingira salama.
“Licha ya kuwapatia elimu mafundi tumeona pia tutoe elimu hii katika Shule za Msingi kwani tunaamini tabia huanza kujengwa toka mtoto anapokuwa mdogo. Hii inamaana kuwa watoto watakapopata elimu hii ya matumizi ya vyoo hivi kuanzia shuleni watakuwa ni mabalozi wazuri katika kaya zao. Kwa upande wa wanafunzi wa Shule za Msingi tunaamini ni rahisi kwao kuendeleza matumizi ya choo bora tangu wakiwa na umri mdogo.”Alisema Mbowe
Kwa upande wake Afisa Afya Halmashauri ya Mji Njombe Saimon Ngassa amesema kuwa madhumuni ya ujenzi wa vyoo kwa kutumia masinki ya plastiki aina ya “SATO” ni muendelezo wa Kampeni mbalimbali za uboreshaji wa Mazingira na kwa sasa Halmashauri inaendelea na Kampeni ya uboreshaji wa vyoo katika maeneo ya Taasisi na Kaya ambapo kwa sasa kampeni hiyo imelenga kuboresha vyoo vya asili kwa kuviwekea masinki ya vyoo vya plastiki na yanayoendana na mazingira halisi.
“Tumejifunza kuwa vyoo hivi vinatumia maji kidogo na ufanisi wake ni mkubwa katika kuzuia harufu na wadudu wanaoingia kwenye vyoo na kwenda kwenye makazi jambo litakaloweza kupunguza maradhi kwa kiasi kikubwa lakini pia ni vyoo vyenye gharama nafuu kwa Wananchi wenye kipato cha chini.”Alisema Ngassa.
Aliendelea kusema “Kampeni hiyo inatekelezwa kwa kuwajengea uwezo mafundi wa eneo husika ambapo kila Kijiji kilitoa fundi mmoja kwa ajili ya kupatiwa mafunzo ili wawewatekelezaji katika kuboresha na kuwajengea vyoo bora Wananchi ngazi ya kaya.”
Johnson Joseph, Bisaya Musa Wanafunzi kutoka shule ya Msingi Kisilo kwa pamoja wanasema kuwa changamoto iliyokuwepo katika vyoo vya mashimo ni uwepo wa harufu kali na wadudu kutoka chooni kusambaa jambo ambalo limepatiwa ufumbuzi kupitia vyoo vipya na wamesema kuwa vyoo hivyo vitasaidia kwenye uthibiti wa magonjwa mbalimbali na atawashauri wazazi kuwa na vyoo hivyo
Patrick Mdetele Fundi kutoka Kijiji cha Utalingolo na Kutoka Rocks Mwalongo kutoka Kijiji cha Idihani wamesema kuwa elimu hiyo inamanufaa makubwa kwao hususani kwa Wananchi watakaowahudumia kwani gharama ni nafuu ukilinganisha na masinki ya aina nyingine na uwepo wa mfuniko ni mdhibiti tosha wa uchafuzi wa mazingira kwa njia ya hewa.
Mkoa wa Njombe umepatiwa jumla ya vyoo 1630 ambapo mpaka sasa Shule za Msingi 33 kutoka Halmashauri ya Mji Njombe zimeweza kujengewa vyoo vya masinki ya “SATO” huku Wananchi wakihamasishwa kutumia teknolojia hiyo na kwa wenye uhitaji waweze kuwasiliana na maafisa afya na watendaji wa vijiji,mitaa na Kata husika ili kuweza kufungiwa vyoo hivyo.
Ofisi yetu inapatikana barabara ya Njombe-Songea mtaa wa Mjimwema.
Sanduku la Posta: S.L.P 577
Simu ya Mezani: 026-2968833
Simu ya Mkononi: 026-2968833
Barua Pepe: td@njombetc.go.tz
Haki Miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Njombe