Katika jitihada za kusaidia jamii yenye uhitaji, Septemba 03, 2024 Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Njombe imetoa msaada wa kiti mwendo kimoja (1) kwa watoto wenye ulemavu kwa familia ya Bi.Agneta Mlowe iliyopo kijiji cha Ikisa kata ya Uwemba.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Njombe ,Afisa Ustawi wa Jamii Ndg.Petro Mahanza alieleza kuwa Seriakali imefanya jitihada za haraka mara baada yakuona taarifa ya wahitaji hao kwenye vyombo vya habari hivyo msaada huo ni sehemu ya juhudi za Serikali katika kuboresha hali ya maisha ya watu wenye ulemavu.
Alisisitiza kuwa ni muhimu kwa jamii kuhakikisha kuwa kila mtu anapata fursa sawa ya kushiriki kikamilifu katika shughuli za kijamii bila kujali hali yake ya kimwili.
"Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Njombe Bi.Kuruthum Sadick baada yakupata taarifa ya wahitaji hawa amechukua hatua za haraka nakutoa baiskeli,kwa kuwapa baiskeli hawa wenzetu, tunawapa nafasi ya kuweza kutembea kutoka eneo moja kwenda eneo jingine kwa urahisi.Hii ni hatua muhimu katika kujenga jamii jumuishi ambapo kila mtu anathaminiwa," alisema Petro Mahanza ,Afisa ustawi wa Jamii Halmashauri ya Mji Njombe.
Kwa upande wa familia wanufaika wa msaada huo pamoja nakuanisha mahitaji mengine walitoa shukrani zao kwa Ofisi ya Mkurugenzi na Serikali kwa ujumla kwa kuwafikia huku wakieleza kuwa kiti mwendo hicho kitasaidia kwa kiasi kikubwa kuboresha maisha yao na kuwapa uhuru zaidi.
Tukio hilo lilihudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Diwani wa Viti Maalum Tarafa ya Igominyi Mhe. Mariam Chundu pamoja na wanajamii.
Ofisi yetu inapatikana barabara ya Njombe-Songea mtaa wa Mjimwema.
Sanduku la Posta: S.L.P 577
Simu ya Mezani: 026-2968833
Simu ya Mkononi: 026-2968833
Barua Pepe: td@njombetc.go.tz
Haki Miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Njombe