Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Njombe, Bi. Kuruthum Sadick, amewataka walimu wa shule za msingi na sekondari kuhakikisha wanawajengea uwezo wanafunzi ili wawe na ujasiri wa kujieleza na kutoa taarifa wanapokutana na vitendo vya ukatili wa kijinsia.
Wito huo umetolewa Agosti 14, 2025, wakati akizindua mdahalo wa wazi ulioandaliwa kwa ajili ya kuwapa watoto nafasi ya kuzungumza kwa uhuru kuhusu changamoto zinazohusiana na ukatili wa kijinsia, kujadili mbinu za kuongeza uelewa, kuimarisha ushirikiano katika kupambana na ukatili huo ndani na nje ya shule, pamoja na kuibua mawazo bunifu ya mikakati ya kuzuia na kushughulikia matukio hayo.
“Tunahitaji watoto wetu wawe na ujasiri wa kusema hapana kwa vitendo vya ukatili na wawe tayari kutoa taarifa pale wanapovikuta. Walimu mnapaswa kuwa walezi na mifano ya kuwapa mwelekeo sahihi watoto wetu,” alisema.
Kwa upande wake, Bw. Odilo Msemwa, Mtaalamu wa Elimu ya Kupinga Ukatili wa Kijinsia kutoka Halmashauri ya Mji Njombe, alisisitiza umuhimu wa walimu kushirikiana na jamii katika mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia, hususan katika mazingira ya shule.
Mdahalo huo ulihudhuriwa na walimu na wanafunzi kutoka Shule za Msingi Mji Mwema na Sinai, Shule ya Sekondari Mpechi, Venithe, na Lunyanywi, pamoja na wadau mbalimbali wa elimu. Washiriki walishauriwa kuwa mstari wa mbele katika kulinda haki, usalama, na ustawi wa watoto.
Ofisi yetu inapatikana barabara ya Njombe-Songea mtaa wa Mjimwema.
Sanduku la Posta: S.L.P 577
Simu ya Mezani: 026-2968833
Simu ya Mkononi: 026-2968833
Barua Pepe: td@njombetc.go.tz
Haki Miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Njombe