Disemba 9, 2024, watumishi wa Halmashauri ya Mji Njombe na wakazi wa Njombe Mjini wameadhimisha miaka 63 ya Uhuru wa Tanzania kwa kushiriki katika shughuli mbalimbali za kijamii, zikiwemo kufanya usafi wa mazingira, kutoa misaada kwa wagonjwa wa Kituo cha Afya Njombe Mjini, na kupanda miti katika Shule ya Sekondari Mpechi.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Njombe na wananchi walishiriki shughuli hizo,Twilumba Mwalongo, Afisa Tawala Halmashauri ya Mji Njombe, aliwasihi wananchi kuendelea kudumisha amani na mshikamano kutoka kwa waasisi wa Taifa la Tanzania.
“Siku kama ya leo inatukumbusha jinsi waasisi wetu walivyolipigania Taifa hili. Ni wajibu wetu kuhakikisha tunadumisha amani na mshikamano kwa manufaa ya kizazi kijacho,” alisema Mwalongo.
Aliongeza kuwa misaada iliyotolewa kwa wagonjwa katika Kituo cha Afya Njombe Mjini ni njia ya kuwafariji wale ambao, kutokana na changamoto za kiafya, hawakuweza kushiriki maadhimisho hayo.
Kwa upande wake, Kaimu Afisa Mtendaji wa Kata ya Njombe Mjini, Nicodemus Funi, alieleza kuwa maadhimisho ya Uhuru katika kata hiyo yamejikita katika kufanya usafi wa mazingira kwa siku kumi katika mitaa yote tisa ya Njombe Mjini.
Shughuli hizo zinalenga siyo tu kuboresha mazingira bali pia kuimarisha mshikamano wa jamii kwa kushirikiana katika kazi za maendeleo.
Ofisi yetu inapatikana barabara ya Njombe-Songea mtaa wa Mjimwema.
Sanduku la Posta: S.L.P 577
Simu ya Mezani: 026-2968833
Simu ya Mkononi: 026-2968833
Barua Pepe: td@njombetc.go.tz
Haki Miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Njombe