Ni katika Mkutano wa mwaka wa baraza la Waheshimiwa Madiwani wa Halmashauri ya Mji Njombe ambapo, Mbunge wa jimbo la Njombe Mjini Mheshimiwa Deo Mwanyika amewataka Wananchi waliopo katikati ya Mji Njombe kuhakikisha kuwa wanazingatia mpango kabambe wa Halmashauri kwenye ujenzi wa nyumba ili kuifanya Halmashauri ya Mji Njombe kukidhi vigezo vya kuwa Manispaa.
Mwanyika amesema kuwa licha ya kuwa kumekuwa na maboresho ya ujenzi katika maeneo mengi hususani katikati ya Mji, lakini bado Wananchi wengi wamekuwa hawazingatii mpango kabambe wa Mji kwani ujenzi ambao umekua ukiendelea kufanyika ni ujenzi wa nyumba za kawaida na sio ujenzi wa maghorofa kama ilivyoainishwa katika mpango huo wa ujenzi katikati ya Mji.
“Bado kwenye maeneo yetu ya Mji Ujenzi unaofanyika sio wa magorofa, ujenzi unaofanyika ni wa kizamani jambo ambalo litaweza kutuchelewesha kupata Manispaa.”Alisema Mheshimiwa Mbunge.
Akizungumza katika mkutano wa Baraza la Mwaka la Waheshimiwa Madiwani Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Njombe Mheshimiwa Erasto Mpete amewapongeza Wataalamu, na Waheshimiwa Madiwani kwa kuiwezesha Halmashauri katika mwaka wa fedha 2021-2022 kukusanya kwa asilimia 141.9 za makusanyo ya ndani jambo ambalo litaiwezesha Halmashauri kutekeleza miradi mingi ya maendeleo.
Wakitoa maoni yako katika mkutano huo baadhi ya Waheshimiwa Madiwani Edwin Mwanzinga Diwani wa Kata ya Matola amesema kuwa licha ya kuwa jitihada kubwa zimefanyika za ukusanyaji mapato lakini bado usimamizi madhubutu unahitajika katika matumizi ya fedha zinazokusanywa ili kuweka nidhamu ya fedha hizo lakini pia kuepuka upanuzi wa vifungu kutokana na bajeti zilizokuwa zimepangwa kushindwa kufikia malengo yaliyokusudiwa.
Naye Diwani wa Kata ya Ramadhan Nickson Nganyange amesema bajeti ya mwaka 2021/2022 imekua ni ya mafanikio makubwa kwani imeweza kufanikisha utekelezaji wa miradi mingi ya maendeleo jambo ambalo limeiletea heshima Halmashauri
Michael Uhaula Diwani wa Kata ya Yakobi amesema kuwa mafanikio yaliyofikiwa katika Kata yake ni pamoja na kufanikisha kuanza kwa kidato cha tano katika shule ya Sekondario Yakobi na pia amewashukuru Wananchi wa Yakobi kwa kuendelea kuchangia kwenye utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Awali Baraza hilo lilitanguliwa na uchaguzi wa Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ambapo Mheshimiwa Filoteus Mligo Diwani wa Kata ya Lugenge alichaguliwa kwa kura za ndio 14 kati ya kura 14 zilizopigwa na hivyo kuidhinishwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri kwa kipindi cha mwaka 2022-20223. Aidha Baraza hilo lilifanikiwa kufanya uchaguzi wa Wenyeviti na kuunda kamati za kudumu za Halmashauri, Bodi ya Ajira na ALAT pamoja na kupitia na kuidhinisha ratiba ya vikao mbalimbali vya Kisheria.
Ofisi yetu inapatikana barabara ya Njombe-Songea mtaa wa Mjimwema.
Sanduku la Posta: S.L.P 577
Simu ya Mezani: 026-2968833
Simu ya Mkononi: 026-2968833
Barua Pepe: td@njombetc.go.tz
Haki Miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Njombe