Rai hiyo imetolewa wakati wa ziara ya Kamati ya Siasa Wilaya ya Njombe yenye lengo la kuangazia utekelezaji wa Ilani ya CCM ambapo walitembelea na kukagua ujenzi wa vyumba vya madarasa katika Kata tatu za Njombe Mjini, Mjimwema na Ramadhani ujenzi unaotekelezwa kupitia fedha za mapambano dhidi ya Uviko, na ambao kutokana na maelekezo ya Serikali ujenzi huo unatakiwa kukamilika kufikia desemba 15 mwaka huu.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo Mwenyekiti wa Kamati Edward Mgaya amesema kuwa kwa kipindi kilichosalia ni vyema nguvu kubwa ya ujenzi iongezwe ili miradi hiyo iweze kukamilika kwa mujibu wa maelekezo ya Serikali na amewataka Wenyeviti wa Mitaa na Watendaji kuhakikisha kuwa wanawahamasisha Wananchi kwa kupangiana zamu kushiriki kwenye kusaidia shughuli za ujenzi ili kuongeza nguvu kazi na kasi kwenye miradi hiyo.
“Muda uliobaki si rafiki, katika maeneo mengine ya Wilaya ya Njombe tumeona ushiriki mkubwa wa Wananchi katika eneo la ujenzi kuhakikisha kuwa miradi hii inakamilika. Katika Kata hizi za Mjini naona kunachangamoto ya ushiriki wa Wananchi. Tukiwategemea mafundi pekee hatuwezi kukamilisha hili kwa wakati. Wananchi wanapaswa kufahamu kuwa wanawajibika katika kusaidia kwani fedha hizi za ujenzi zisingeletwa na Serikali Wananchi wangepaswa kuchanga kujenga madarasa. Sasa tumeletewa fedha za ujenzi kwanini wasisaidie? Miradi tunataka ikamilike kufikia tarehe 15 na kwa ubora hivyo wekeni mikakati mizuri ya kufanikisha hili.”Alisema Mgaya
Katika hatua nyingine wajumbe wa kamati hiyo wamelaani vikali tukio lililofanywa na Wananchi wasio wema kwenye Kata ya Mjimwema kwa kuvunja masinki ya vyoo 11katika Shule mpya ya Mjimwema jambo lilaloitia hasara Serikali lakini pia kuwaongezea mzigo Wananchi kuchangia tena kununua masinki mapya ili kurejesha katika vyoo vyote ambavyo masinki yake yaliharibiwa.
Kwa upande wake katibu wa CCM Wilaya ya Njombe Sure Mwasanguti amepongeza kasi ya ujenzi katika Shule ya Sekondari Mpechi ambayo kwa sasa ipo katika hatua ya upigaji wa lipu na ameupongeza Mtaa wa Kambarage kwa kujitoa kuchangia ujenzi wa Shule mpya ya msingi Kambarage B ambapo kwa kiasi kikubwa shule hiyo itasaidia kupunguza msongamano wa Wanafunzi katika shule ya Kambarage.
“Kwenye fedha tulizopewa na Serikali tunahitaji kila kitu kikimbie. tunapokimbiza maendeleo yanaisha vizuri ila tunapochelewesha tunabaki palepale. Mji wetu hauwezi kukuwa kama tusiposhirikiana kwa pamoja” Alisema Mwasanguti.
Licha ya Kamati kukagua miradi 3 ya vyumba vya madarasa vyenye thamani ya shilingi milioni 360 ikiwa ni fedha za mapambano ya UVIKO,ukaguzi mwingine ni ujenzi wa Shule mbili mpya za msingi ujenzi unaofanywa na nguvu za Wananchi,wadau na Halmashauri na ujenzi wa kituo kipya cha Afya Mjimwema ambacho kitasaidia kupunguza msongamano wa wagonjwa katika kituo cha Afya Njombe Mjini.Pia Kamati hiyo pia imekagua shughuli za Kilimo cha miche ya parachichi kinachofanywa na moja ya kikundi cha Wanawake Mjimwema kikundi kilichopatiwa milioni 10 kutoka kwenye asilimia kumi ya mikopo ya Wanawake,Vijana na Walemavu na kufurahishwa na shughuli yao kwani thamani ya fedha na mradi unaoendelea vinatija iliyokusudiwa.
Aidha.Kamati hiyo imekagua ujenzi wa Daraja linalounganisha Kata ya Ramadhani na Njombe Mjini na ujenzi wa Barabara ya lami katika Mtaa wa Idundilanga ujenzi unaotekelezwa na Wakala wa barabara Vijijini na Mjini Wilaya ya Njombe (TARURA) .
Halmashauri ya Mji Njombe imepokea kiasi cha Shilingi milioni 740 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba 37 katika shule 12 za Sekondari na shilingi milioni 80 ikiwa ni ujenzi wa bweni la Wanafunzi wenye mahitaji maalumu katika Shule ya Msingi Kibena na hivyo kufanya jumla kuu ya fedha zilizopokelewa kuwa shilingi milioni 820 hii ikiwa ni fedha za mapambano ya UVIKO 19.
Ofisi yetu inapatikana barabara ya Njombe-Songea mtaa wa Mjimwema.
Sanduku la Posta: S.L.P 577
Simu ya Mezani: 026-2968833
Simu ya Mkononi: 026-2968833
Barua Pepe: td@njombetc.go.tz
Haki Miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Njombe