Wananchi wa Kata ya Kifanya, Halmashauri ya Mji Njombe, wameishukuru Serikali kwa kuwajengea kituo cha afya chenye miundombinu na vifaa vya kisasa, ambacho kitawasaidia kuondokana na tatizo la kutembea umbali wa kilomita 50 kwenda hospitali ya Kibena Mjini Njombe kwa ajili ya huduma za afya.
Wakizungumza Septemba 11, 2024 mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), iliyotembelea kituo cha afya cha Muungano kilichopo Kata ya Kifanya, wananchi hao walieleza kuwa awali walilazimika kusafiri umbali mrefu kupata huduma za afya, lakini sasa hali imebadilika kwa sababu wanapata huduma hizo karibu.
"Tulilazimika kusafiri hadi hospitali ya Kibena au Ikonda iliyopo wilaya ya Makete, ambako ni mbali sana. Tunaishukuru sana Serikali kwa kuboresha huduma za afya na kujenga majengo mapya," alisema Romanus Tweve, mmoja wa wananchi.
Diwani wa Kata ya Kifanya, Mheshimiwa Nolasco Mtewele, alieleza kuwa ujenzi wa kituo hicho ulianzishwa na wananchi wenyewe, na baadaye Serikali kupitia mapato ya ndani ya Halmashauri ilileta fedha zaidi ya milioni 500 kwa ajili ya kukamilisha mradi huo.
"Naomba mtufikishie salamu zetu za shukrani kwa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutupatia fedha na vifaa tiba kwa ajili ya kituo hiki," Alisema Mhe.Mtewele.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya TAMISEMI, Justine Nyamoga, aliipongeza Serikali kwa kuendelea kuboresha huduma za afya mijini na vijijini.
"Sisi kama Bunge tumeridhishwa sana na utekelezaji wa miradi tunayokutana nayo. Kituo hiki cha afya Muungano Kifanya ni mfano wa uboreshaji wa huduma za afya katika maeneo ya vijijini. Tumeona chumba cha upasuaji ambacho kinaendana na viwango vya kisasa sawa na vile vilivyopo katika hospitali kubwa," Alisema Mhe.Nyamoga.
Jumla ya muondombinu mipya sita (6) imejengwa katika kituo cha afya Muungano Kifanya ambayo ni, Jengo la mama na mtoto,Mionzi,maabara,jengo la kufulia, jengo lakuhifadhia maiti,jengo la upasuaji pamoja na Njia (walkways).
Ofisi yetu inapatikana barabara ya Njombe-Songea mtaa wa Mjimwema.
Sanduku la Posta: S.L.P 577
Simu ya Mezani: 026-2968833
Simu ya Mkononi: 026-2968833
Barua Pepe: td@njombetc.go.tz
Haki Miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Njombe