Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Nchini TASAF kupitia Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini TASAF III Umetoa elimu kwa vikundi 14 vya Wanufaika wa Mpango huo kuhusu uwekaji akiba na kukuzaji uchumi katika Kata za Utalingolo na Uwemba zilizopo katika Halmashauri ya Mji Njombe.
Akizungumza malengo ya elimu ya vikundi kwa wanufaika wa TASAF Afisa Ufuatiliaji Kitengo cha Maendeleo ya Miundombinu TASAF Ndg. Augustino Ngude amesema kuwa lengo kuu la mpango huo ni kukuza utamaduni wa kujiwekea akiba kwa kaya maskini ili kuwawezesha kukabiliana na dharura na mahitaji ya msingi pasipo kutegemea ruzuku ya TASAF.
“Tunatoa elimu hii ya uundwaji wa vikundi na kuweka akiba kwa wanufaika wa Mpango wa kunusuru kaya maskini ili kufanya mradi uwe endelevu. Kila mradi huwa na mwanzo na mwisho ila tunategemea kupitia vikundi ambavyo wameshavianzisha vitawasaidia wanufaika hao hata pale ambapo mradi utakapokuwa umefikia ukomo.”Alisema
Ngude aliendelea kusema “Vikundi 14 tulivyovitembelea kwa siku mbili hizi vimekuwa vikifanya vizuri kwenye kuweka akiba. Yapo maeneo ambayo walikuwa wanakwama kutokana na ukosefu wa elimu ya akiba na utunzaji kumbukumbu za fedha kwenye kikundi .Mafunzo tuliowapatia yamewasaidi kubaini wapi walikuwa wanakosea na namna bora ya kuboresha kile walichoanzisha. Naomba nitoe rai kwa wawezeshaji kuendelea kuvitembelea vikundi hivi mara kwa mara ili kuendelea kutoa elimu zaidi” Alisema
Mark Salema, Henry Kideula, Christina Tsangai na Mariam Monjesa ni Wawezeshaji TASAF Ngazi ya Halmashauri ambao wao kwa pamoja wamepongeza mwitikio wa wanufaika hao kujiunga katika vikundi vya kuweka akiba na kukuza uchumi na kubaini changamoto kubwa inavyovikabili vikundi hivyo kuwa ni ukosefu wa elimu juu ya utunzaji wa kumbukumbu za fedha kwenye kikundi na Wanakikundi kuweka kiwango kikubwa cha akiba ukilinganisha na kipato wanachopata huku muda wa kukutana ukiwa mrefu changamoto inayofanya wanakikundi wengine kushindwa kuendelea na wengine kushindwa kukopa kwa wakati.
Wawezeshaji hao wamesema kuwa kupitia mafunzo hayo wameweza kuwaelekeza wanufaika kuweka akiba kidogo kulingana na kipata chao huku wakiendelea kujishughulisha kwenye miradi midogo midogo itakayowaingizia kipato cha kudumu badala ya kutegemea ruzuku ya TASAF na kuwahamasisha wanakikundi kukutana angalau kila wiki ili kuweza kuwa na taarifa za mara kwa mara za kikundi na pia itasaidia Wanakikundi kukopa na kurejesha kila wakati na kuondokana na kupata faida kidogo wakati wa mgawanyo.
Kwa upande wao Wanufaika wa Mpango huo Bi Foida Samwel kutoka kikundi cha Muungano ambao mpaka sasa kikundi chao kina kiasi cha Shilingi Laki saba na Bi Sixbetha Mpete kutoka kikundi cha Upendo na Kazi ambacho kina zaidi ya Shilingi milioni tatu vyote kutoka Uwemba, wamesema kuwa wanaishukuru TASAF Kwa mafunzo hayo kwani yamezidi kuwapa mwanga wa kuendelea kupambana na umaskini kwa kufanya kazi kwa juhudi na kuweka akiba ili kuendelea kuboresha maisha.
Mpaka sasa Halmashauri ya Mji Njombe imefanikiwa kuunda vikundi 123 vya wanufaika katika Kata 13 na imeanza kutoa elimu kwa vikundi 14 katika awamu ya kwanza na inaendelea na zoezi la utoaji elimu ya uwekaji akiba kwa vikundi vilivyosalia ili kuvijengea uwezo zaidi. Ikumbukwe kuwa TASAF II ilionyesha mafanikio makubwa katika kuunda vikundi ambapo vikundi 1172 viliundwaa na kati ya hivyo vikundi 1000 vilipatiwa mafunzo na vifaa kwa ajili ya uwekaji wa akiba kwa vikundi na wanufaika walitumia akiba zao kubadili hali zao za maisha.
Ofisi yetu inapatikana barabara ya Njombe-Songea mtaa wa Mjimwema.
Sanduku la Posta: S.L.P 577
Simu ya Mezani: 026-2968833
Simu ya Mkononi: 026-2968833
Barua Pepe: td@njombetc.go.tz
Haki Miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Njombe