Katika kuadhimisha siku ya Usafishaji Duniani Septemba 16,2023, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Njombe Ndugu Kuruthum Sadick amesema Halmashauri haitamvumilia mwananchi yeyote, atakayeonekana kuchafua mazingira kwa kutupa taka hovyo mitaani na kwenye maeneo yasiyo rasmi.
Akielezea umuhimu wa usafi na kutunza mazingira Mkurugenzi Kuruthum amesema kuwa, usafi ni afya na ukitunza mazingira yanakutunza hivyo kila mwananchi anawajibu wakuhakikisha anafanya usafi kwenye maeneo yanayomzunguka kutunza maeneo ya mabonde na vyanzo vya maji kwa kuacha kutupa takataka hovyo.
Akiwa eneo la bonde linalopita mtaa wa National Housing kata ya Njombe Mjini ,ametoa onyo kwa wananchi ambao wanatupa taka kwenye bonde hilo ambalo siyo dampo rasmi kwa ajili ya takataka nakusema Halmashauri imetenga eneo rasmi kwa ajili ya kutupa taka hivyo bonde hilo lisitumike kutupia taka.
“Tumeweza kujumuika kufanya usafi kwenye hili bonde ni wasihi wananchi kuacha kutupa taka kwenye bonde hili na yeyote atakayebainika hatua kali zitachukuliwa,na tufahamu kuwa kuna vyanzo vyanzo vya maji kwenye bonde hili na tunaelekea msimu wa mvua siyo afya kwa vyanzo vyetu vya maji maana maji haya yanatumika, Halmashauri ina magari yakukusanya taka kupeleka dampo tuache kabisa kutupa taka kwenye eneo hili ambalo siyo rasmi ”
Katika hatua nyingine amesema ili kuhakisha Mji wa Njombe unaendelea kubaki katika hali ya usafi ,Halmashauri ya Mji Njombe itaendelea kuhamasisha na kushiriki usafi wa pamoja kila mwezi ili kuwa kumbusha wananchi kuwa wanawajibu wakutunza mazingira na kufanya usafi mpaka kwenye maeneo yanayowazunguka majumbani.
“Usafi usiishie hapa tu,tufanye usafi hadi majumbani, hii itatukinga na magonjwa, kama kipindupindu”
Kwa upande wake Afisa Afya wa Mkoa wa Njombe Bi.Saada Milanzi amesema ili kuendelea kutunza mazingira Halmashauri zote za mkoa wa Njombe ziendelee kutumia sheria ndogo zilizopitishwa ili kuwawajibisha na kudhibiti utupaji taka kwenye maeneo yasiyo rasmi.
Aidha ametoa wito kwa wananchi kuitikia wito wakushishiriki shughuli za usafi na kutii sheria mbalimbali za usafi na utunzaji wa mazingira zilizowekwa na Halmashauri ili kuweka mazingira safi na kuzuia magonjwa ya mlipuko .
Naye mtendaji wa kata ya Njombe Mjini Enos Lupimo ameeleza mikakati waliyonayo katika kuweka eneo la Mji safi pamoja na kupambana na utupaji wa taka hovyo kwenye maeneo yasiyo rasmi kama kwenye mabonde.
“Sisi kama kata tunaenda kuunda kikosi kazi ambacho kitafanya kazi kuanzia ngazi ya mtaa ,kitahusu mazingira na afya,tutaoa elimu ya usafi na utunzaji wa mazingira na kisha tutaanza kuchukulia hatua wananchi ambao watakiuka sheria nakutupa taka hovyo kwenye mabonde na mitaani,tutakuwa na walinzi kwenye haya mabonde watafanya kazi usiku na mchana ,na ukionekana unatupa taka hovyo faini itahusika kwa mujibu wa sheria”.
Wadau mbalimbali ambao wameshiriki kuadhimisha siku hii ikiwemo taasisi ya SHIPO , Benki ya Taifa ya Uchumi (NBC),wanafunzi pamoja na vikundi vya vijana vinavyojishughulisha na mazingira ,wamesema jamii inatakiwa kutambua kuwa taka ni mali hivyo wanaweza kuzikusanya kwa utaratibu wakuzitenga taka ngumu zisizooza kama vile chupa za plastiki na zikatumika kwenye utengenezaji wa bidhaa mbalimbali.
Halmashauri ya Mji Njombe kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa mazingira pamoja na wananchi imeungana na nchi mbalimbali Duniani kuadhimisha siku ya usafishaji duniani kwa kufanya usafi kwenye maeneo mbalimbali ya Mji wa Njombe .
MATUKIO KATIKA PICHA
Ofisi yetu inapatikana barabara ya Njombe-Songea mtaa wa Mjimwema.
Sanduku la Posta: S.L.P 577
Simu ya Mezani: 026-2968833
Simu ya Mkononi: 026-2968833
Barua Pepe: td@njombetc.go.tz
Haki Miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Njombe