Halmashauri ya Mji Njombe imejizatiti kukusanya mapato kwa kutatua changamoto ya upungufu wa vitendea kazi kwa watendaji wa Kata katika Halmashauri hiyo.
Akizungumza wakati wa makabidhiano ya pikipiki hizo kwa watendaji wa Kata za Lugenge, Matola, Ihanga na Kifanya Mkuu wa Idara ya Utumishi na Utawala Halmashauri ya Mji Njombe Abdulatif Mkata amesema kuwa lengo la Halmashauri kuwakopesha pikipiki hizo ni kutoa motisha kwa watendaji waliofanya vizuri katika utendaji wao wa kazi na kurahisisha utendaji kazi wa watendaji hao wa Kata kwa kuwa Kata wanazozisimamia ni kubwa na pikipiki hizo zitawawezesha kutekeleza majukumu yao kwa urahisi kwa kuweza kufika kwenye Vijiji vya Kata na kufanikisha utoaji wa huduma kwa jamii kwa wakati.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Njombe Edwin Mwanzinga amewataka watendaji hao kuhakikisha kuwa wanazitunza pikipiki hizo na kuhakikisha kuwa zinatumika kwa ajili ya ufuatiliaji wa mapato ya Halmashauri na usimamizi wa shughuli za maendeleo katika Kata zao.
“Kwanza natoa pongezi kwa kazi nzuri mlizofanya katika Kata zenu. Pikipiki hizi tumewapatia ili ziwasaidie katika utekelezaji wa shughuli zenu za kila siku. Ni matumaini yangu kuwa sasa mtaenda kusimamia shughuli za maendeleo ya Kata kwa urahisi lakini kubwa zaidi kusimamia mapato ya Halmashauri kikamilifu.”Alisema Mwanzinga.
Khadija Lutumo ni Mtendaji wa Kata ya Lugenge Halmashauri ya Mji Njombe ambaye ni miongoni mwa watendaji waliokabidhiwa pikipiki hizo ambapo ameishukuru Halmashauri kwa kutoa motisha ya pikipiki kwani itasaidia kutatua changamoto ya uhaba wa vitendea kazi na ameahidi kuendelea kufanya kazi kwa bidii katika Kata yake na kusimamia mapato kikamilifu kwani kwa kutumia pikipiki aliyokabidhiwa swala la usimamamizi litakuwa rahisi.
Halmashauri ya Mji Njombe imefanikiwa kununua pikipiki nne zenye thamani ya Shilingi milioni tisa laki 4 kupitia mapato ya ndani na imekusudia kuhakikisha kuwa katika siku za mbeleni watendaji wote watakaofanya vizuri katika maswala ya utendaji kazi na ukusanyaji mapato wanakopeshwa pikipiki kwa kutenga bajeti na kuhakikisha Mazingira ya kazi ya watumishi wake yanaboreka siku hadi siku.
Ikumbukwe kuwa Halmashauri ya Mji Njombe ni miongoni mwa Halmashauri za Miji zinazofanya vizuri katika swala la ukusanyaji mapato na imejizatiti kuhakikisha kuwa kadri siku zinavyosonga mbele ikusanye zaidi ya malengo yaliyokusudiwa na kuibuka kinara katika makusanyo ya mapato.
Ofisi yetu inapatikana barabara ya Njombe-Songea mtaa wa Mjimwema.
Sanduku la Posta: S.L.P 577
Simu ya Mezani: 026-2968833
Simu ya Mkononi: 026-2968833
Barua Pepe: td@njombetc.go.tz
Haki Miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Njombe