Tarehe 16 Disemba 2024 Afisa Ustawi wa Jamii wa Halmashauri ya Mji Njombe, Vickiana Kiwelu, ametoa wito kwa wazazi na walezi kuhakikisha wanalinda watoto wao dhidi ya ukatili wa kijinsia wakati wa msimu wa Sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye Ofisi ya Mtaa wa Lunyanywi, Kiwelu alisisitiza umuhimu wa jamii kuwa mabalozi wa kupinga ukatili dhidi ya watoto. Alihimiza pia wananchi kuheshimu utu na kuepuka kujichukulia sheria mkononi wakati changamoto zinapojitokeza.
"Niwaombe wananchi, katika kipindi hiki cha sikukuu, tuwalinde watoto wetu. Tunapopokea wageni majumbani mwetu, si kila mtu anakuja kwa nia nzuri. Kama nyumba yako ni ndogo na unalazimika kumpa mgeni hifadhi, tafuta mahali pa kumpeleka mbali na watoto ili kuwaepusha na hatari ya ukatili," alisema.
Aliongeza kuwa wazazi wanapaswa kuwa waangalifu, hasa wakati wa msimu wa sikukuu ambapo mara nyingi hutembelewa na ndugu na marafiki. Alikumbusha kuwa baadhi ya watu hujificha nyuma ya uhusiano wa kifamilia huku wakiwa na nia mbaya.
Aidha, alizungumzia changamoto ya wazazi waliotengana kutotimiza wajibu wa kuwalea watoto wao, akibainisha kuwa kumekuwa na ongezeko la akina mama kufika ofisi za serikali kudai matunzo kutoka kwa wenza wao.
"Naomba wazazi wote, hasa wale waliotengana, wahakikishe wanatimiza wajibu wao wa kuwalea watoto. Watoto wanahitaji matunzo na malezi bora, si jukumu la mama peke yake au baba peke yake," aliongeza.
Wito huo umelenga kuhimiza wazazi na jamii kwa ujumla kuchukua hatua za tahadhari ili kuhakikisha watoto wanalindwa na kupatiwa mazingira salama, hasa katika msimu huu wa sikukuu unaohusisha mwingiliano mkubwa wa kijamii.
@ortamisemi @maendeleoyajamii @kissagwakisakasongwa @njombe_rs
Ofisi yetu inapatikana barabara ya Njombe-Songea mtaa wa Mjimwema.
Sanduku la Posta: S.L.P 577
Simu ya Mezani: 026-2968833
Simu ya Mkononi: 026-2968833
Barua Pepe: td@njombetc.go.tz
Haki Miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Njombe